WANANCHI WAISHIO PEMBEZONI MWA MJI WA BUKOBA WAOMBA PUNGUZO ADA YA TAKA.
Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Wananchi waishio pembezoni mwa mji wa Bukoba mkoani Kagera wameiomba serikali kuwapunguzia gharama za ada ya taka kutokana uzalishaji wa taka katika maeneo yao kuwa mdogo.
Wakizungumza na Matukio Daima Media wananchi hao akiwemo Poul Gerevas mkazi wa Omukibeta kata ya Kibeta amesema kuwa taka anazozalisha anazitupa shambani kwake hivyo haoni sababu ya kulipa ada ya taka, huku hata akilipa wanaochukua taka hawafiki kwakwe.
"mimi ninalipa ushuru wa taka ila silidhishwi nao, kwa upande wangu ninapoishi gari la taka halifiki ila wanaozoa taka wanafika kudai ushuru wa taka, lakini pia sehemu ninapoishi nina shamba hivyo taka ninazozalisha naziweka shambani kama mbolea kwahiyo sioni sababu ya kulipa Ada ya taka".
Naye Victor Salestin ametaka kulipa ushuru wa taka kulingana na taka anayozalisha, tofauti na sasa kuwekewa kiwango kwa watu wote kwa wanaofanya biashara kubwa na ndogo na kupelekea mtu kulipa kiwango kikubwa cha fedha tofauti na taka anazozalisha.
"tunaiomba serikali na wote wanaohusika na ukusanyaji wa taka wawe wanaangalia na kiwango cha uzalishaji taka, wamtoze mtu hela kulingana na kiwango anachozalisha taka".
Katika hatua nyingine Bw.Victor ameiomba serikali na maafisa Afya kutoa elimu kwanza kwa wananchi juu ada ya taka inaenda kufanya nini kabla ya kuanza kukusanya ushuru huo.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha usimamizi wa taka manispaa ya Bukoba Tambuko Joseph amesema kuwa ada ya taka inalipwa kulingana na aina ya biashara na aina kaya katika maeneo katikati ya mji na pembezoni mwa mji.
"kwa mujibu wa sheria ndogo ya mwaka 2018 Ada ya taka inalipwa kulingana na aina ya biashara na aina ya makazi kwa mfano kaya za mjini Ada ni shilingi 1,000 na kaya za pembezoni ni shilingi mia tano kwa mwezi".
Hata mkuu huyo wa kitengo cha usimamizi wa taka amewataka wananchi katika manispaa ya Bukoba kuendelea kulipa Ada ya taka ili kusaidia mkandarasi anayehusika kukusanya taka atimize majukumu yake.



