Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI WA MTAA CHINYOYO WACHIMBA MSINGI WA OFISI YA SERIKALI KWA NGUVU ZAO

WANANCHI WA MTAA CHINYOYO WACHIMBA MSINGI WA OFISI YA SERIKALI KWA NGUVU ZAO


Na Matukio Daima Habari Dodoma

WANANCHI wa Mtaa wa Chinyoyo, Kata ya Kilimani, Jijini Dodoma wameanza rasmi ujenzi wa ofisi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwa kuchimba msingi wa jengo hilo leo, hatua inayotajwa kuwa mwanzo wa kutatua changamoto ya muda mrefu ya kukosekana kwa ofisi rasmi ya mtaa.

Kwa miaka kadhaa, wananchi wa mtaa huo walilazimika kumfuata Mwenyekiti nyumbani kwake au kwenda katika ofisi ya Mtendaji wa Kata iliyopo mtaa mwingine ili kupata huduma. 

Hali hiyo imekuwa ikiwasababishia usumbufu na gharama za ziada za usafiri, hususan kwa kutumia bodaboda au bajaji.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chinyoyo, Mhe. Faustina Bendera, amesema kukosekana kwa ofisi kulikuwa kikwazo kikubwa katika utoaji wa huduma.

“Wananchi walikuwa wanakuja nyumbani hata wakati wa shughuli binafsi.

Ilibidi nisimamishe kazi za nyumbani ili kuwasikiliza na wakati mwingine kuambatana nao kufuatilia changamoto zao,” amesema.

Ameongeza kuwa hata watendaji wa mtaa walikuwa wakifanya kazi katika mazingira yasiyo rafiki kwa kukosa ofisi, jambo lililolazimu baadhi ya huduma kutolewa katika ofisi ya kata. 

Ujenzi wa jengo hilo sasa utawezesha Mwenyekiti na Mtendaji wa Mtaa kupatikana sehemu moja na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Mradi huo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi wenyewe baada ya makubaliano ya kila kaya kuchangia shilingi elfu tano.

Inakadiriwa kuwa kaya takribani 3,000 zikikamilisha mchango huo, zaidi ya shilingi milioni 15 zitakusanywa kusaidia hatua za awali za ujenzi.

Mbali na michango ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe.
Anthony Mavunde, ametoa msaada wa matofali ya block 1,000 pamoja na mifuko 50 ya saruji ili kuunga mkono juhudi hizo.

Diwani wa Kata ya Kilimani, Mhe. Mussa Mkunda, amewapongeza wananchi kwa moyo wao wa kujitolea na kuahidi kushirikiana nao hadi ujenzi utakapokamilika.

 Amesema atahakikisha anaisemea hoja hiyo katika Halmashauri ya Jiji ili kupata msaada zaidi pale utakapohitajika.

Kuanzishwa kwa ujenzi wa ofisi hiyo kunatajwa kuwa ni hatua muhimu ya kusogeza huduma za serikali karibu na wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na uongozi wa mtaa.

Mwisho





 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3