WANANCHI WA MBOLIBOLI WALALAMIKA UCHELEWESHAJI UJENZI WA SKIMU YA UMWAGILIAJI MKOMBOZI WASEMA MUDA WA KILIMO CHA MPUNGA UNAISHIA
NA ANGELINA MBUNDA (Uol),MATUKIO DAIMA MEDIA -0754026299
WANANCHI wa Kata ya Mboliboli, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa wamlalamikia mkandarasi anayejenga mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi kuchelewesha ukamilishaji wa mradi huo huku msimu wa Kilimo cha Mpunga ukifika ukingoni.
Wananchi hao waliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, wakimtaka Mhandisi wa mradi pamoja na wakandarasi wake kuhakikisha mfereji wa maji inayotoka T13 hadi T16 inarekebishwa haraka ili kuruhusu upatikanaji wa maji mashambani.
Kwa mujibu wa wananchi, hadi sasa bado hawajaotesha mpunga huku muda wa kupandikiza ukikaribia kuisha, jambo linalozua hofu ya kupoteza mbegu na kuathiri maisha yao ya kiuchumi.
“Tunahitaji mifereji itengenezwe na maji yapite kutoka T13 hadi T16. bila maji hatuwezi kulima mpunga. Kila siku tunaahidiwa lakini utekelezaji hatuuoni. Kama hatutalima, tutaishi vipi?” walilalamika wananchi kwa pamoja.
Diwani wa Kata ya Mboliboli, Yusufu Msamba, alisema hali hiyo ni ya kutia wasiwasi na akamtaka Mhandisi wa mradi kuchukua hatua za haraka kabla wananchi hawajapata hasara kubwa.
“Serikali imekuamini ukaja kutekeleza mradi huu, hivyo ni muhimu ahadi zako zitekelezwe kwa wakati. Mimi niko tayari kushirikiana nawe na tutaweka kambi hapa hadi pale mradi utakapokamilika,” alisema Diwani Msamba.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo alisema kuwa maandalizi ya kukamilisha kazi yanaendelea na kwamba wamekubali kuweka kambi katika eneo hilo ili kuongeza kasi ya utekelezaji.
“Baada ya siku chache mradi huu utakuwa umekamilika. Tutaweka kambi hapa na kufanya kazi kwa ufanisi ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa Mboliboli,” alisema mkandarasi.
Huku Mhandisi wa mradi, Peter Akonai, aliwaomba wananchi kuwa na subira akiahidi kukamilisha marekebisho ya mifereji yote iliyosalia ndani ya muda mfupi.
“Ninawaahidi baada ya siku chache mifereji itakuwa imekamilika na mtapata amani ya kuendelea na kilimo cha mpunga. Kulima siyo kumwagilia, hata mimi nisingeweza kuvumilia hali hii. nipo tayari kuweka kambi hapa pamoja na wakandarasi hadi kazi ikamilike,” alisema Mhandisi Akonai.
Afisa tarafa ya Pawaga Emmanuel Ngabuji aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa watulivu na kuwa malalamiko yao yatafanyiwa kazi.
Pamoja na kuwaomba wananchi kuwa watulivu pia alionya baadhi ya wakulima wa mtama ambao wanavunja taratibu na kwenda kupanda mtama eneo la wafugaji kuacha mara moja na wafugaji wanaopitisha mifugo kwenye tuta la mfereji wa umwagiliaji kuacha vinginevyo mkandarasi anaruhusiwa kukamata mifugo hiyo .
Mradi huu wa unajengwa na kampuni ya COMFIX AND Engineering Company na CRJE Chinese EAST Africa Company,mradi huu wa Mkombozi unanufaisha kata mbili za Mboliboli na Itunundu ambapo walengwa zaidi 20,000 watanufaika,mradi huu asilimia 80 upo kata Mboliboli na asilimia 20 upo kata ya Itunundu na una jumla ya Hekari 15,0000 utajengwa kwa Tsh Bilioni 56 fedha kutoka Serikaki kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
Sehemu ya Mfereji iliyojengwaUjenzi wa mradi wa mfereji wa Mkombozi Pawaga
Sehemu ya Mfereji inayolalamikiwa wa wananchi Waandishi wa Matukio Daima Media wakiwa Pawaga kufuatilia kero za wananchi









