WANANCHI BUKOBA, WAJITOLEA KUTENGENEZA BARABARA
Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Wananchi wa Kitongoji cha Mwizi kijiji Kilima kata Nyakato halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameamua kujitolea kutengeneza barabara ambayo inakatiza katika kitongoji chao kutokana na ubovu wa barabara hiyo ambao mara nyingi umepelekea kukwama kuzifikia huduma muhimu za afya pamoja na elimu kwa wanafunzi.
Wakizungumza mara baada ya kutengeneza Barabara hiyo wananchi hao akiwemo Anastella Kyaruzi amesema kuwa ubovu wa barabara hiyo umekuwa ukipelekea baadhi watoto kushindwa kufika shuleni hasa nyakati za mvua kutokana na Barabara hiyo kujaa maji.
“changamoto tuliyonayo katika kitongoji hiki ni ubovu wa barabara hii, watoto wetu wanashindwa Kwenda shuleni barabara inajaa maji hasa nyakati za mvua inatulazima mpaka kuwabeba kuwapeleka shule”.
Naye Traiphon Mwanuzi ameiomba serikali kuwakumbuka na kuwatengenezea Barabara angalau kiwango cha changalawe ili kuwapunguzia adha usafiri na usafirishaji.
“tunaomba serikali walau itukumbuke ituletee japo kifusi ili kutuondolea hii changamoto ya ubovu wa barabara na kupelekea kushindwa kupitika hasa wakati wa mvua”.
Naye diwani wa kata ya Nyakato Richard Mwombeki ameuomba wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA, kuwawekea karavatiki katika maeneo korofi na pia ameomba barabara korofi kuziweka katika bajeti za kila mwaka ili ziwe zinafanyiwa marekebisho.
“niwombe watu wa TARURA watuwekee makaravati katika maeneo korofi, na pia naomba barabara hizi walau kila mwaka kuziweka katika bajeti, watengeneze vipande vipande kusudi watu wasikwame”.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Bukoba, Mhandisi Emmanuel Festo amesema kuwa tayari wamepokea hitaji la wananchi hao na wameanza hatua za awali za kumwaga kifusi na wameiweka kwenye bajeti yam waka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya matengenezo.
“sisi kama TARURA tumechukua hatua ya kuiingiza barabara hiyo kwenye mpango wa matengenezo lakini kwa vile eneo hilo halipitiki tunafanya juhudi na mheshimiwa diwani wa eneo hilo kuhqkikisha barabara ili inapitika kwa kumwaga kifisi cha changalawe na kurekebisha eneo lile na tumeo lita mia moja za mafuta ili kupeleka kifusi hicho”
Katika mwaka wa fedha wa 2026/2027 jumla ya shilingi milioni 267 zimepangwa kutumika katika matengenezo ya Barabra katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.




