UMUHIMU WA KUMPELEKA MTOTO SHULE KATIKA UMRI MDOGO
Na Angelina Mbunda, MATUKIO DAIMA (UoI)
Baadhi ya walimu na wazazi katika Kata ya Kihesa, mkoani Iringa, wameeleza faida za kuwapeleka watoto shule katika umri mdogo, hususan kuanzia miaka miwili na kuendelea, wakisema hatua hiyo huchangia ukuaji mzuri wa mtoto kiakili na kijamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walimu na wazazi hao wamesema kuwa watoto wanaoanza shule mapema huwa wepesi wa kuelewa masomo darasani na hujenga uwezo mzuri wa kuwasiliana.
Mwalimu wa shule ya awali ya Royal Day Care, Lameck Paulo, amesema kuwa kumpeleka mtoto shule katika umri mdogo humsaidia kuwa mwepesi wa kuelewa mambo mbalimbali pamoja na kujiamini.
“Kunafaida kubwa kumuwahisha mtoto shule katika umri mdogo kwani humfanya awe mwepesi wa kuelewa mambo mbalimbali na kuwa jasiri. Aidha, kama mtoto bado hawezi kutamka maneno vizuri, akichangamana na wenzake hupata uwezo wa kujifunza na kukariri maneno kutoka kwao,” alisema Paulo.
Kwa upande wake, mwalimu Tukuzeni wa Ombeni Nursery School amesema kuwa kuwapeleka watoto shule mapema, hasa katika umri wa miaka mitatu hadi mitano, huchochea ukuaji wao wa kiakili na kijamii.
“Mtoto anayeanza shule mapema huwa mwepesi wa kukariri na kuelewa mambo, anakuwa jasiri na mchangamfu tofauti na yule anayeanza shule akiwa amechelewa,” alisema.
Naye mzazi na mwanaharakati, Emmanuel Msigwa, mkazi wa Semtema, amesema kuwa elimu ya awali ina mchango mkubwa katika kumjenga mtoto kimaadili na kiakili.
“Mtoto anapopelekwa shule mapema hukua vizuri kiakili na kimaarifa, hujifunza maadili ya kuishi na jamii pamoja na kuzoea mazingira ya shule. tofauti na mtoto anayechelewa kuanza shule, ambaye huweza kupata changamoto ya kuzoea mazingira mapya ya masomo,” alisema Msigwa.
Hivyo wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu ya awali na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kuanza masomo katika umri unaofaa ili kuwaandaa vyema kwa hatua zinazofuata za elimu.
