MTOTO EUGENE EVANCE ALIYEIBWA NA BINTI WA KAZI APATIKANA AKIWA HAI ..
Mama Mazazi wa Mtoto Eugene Evance Bi Happines Joshua akiwa amempakata mtoto wake baada ya kumpata akiwa salama.
Mtoto Eugene Evance aliyekuwa ameripotiwa kupotea hatimaye amepatikana akiwa mzima na mwenye afya njema, jambo lililoleta faraja kubwa kwa familia yake na jamii kwa ujumla.
Kuwa mtoto Eugene Evance amepatikana jana Jumamosi huko Kisemvule,Utunge wilaya ya Mkuranga.
Kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo Happines Joshua alisema kuwa tukio hilo lilikuwa la kushtua na la kutia hofu kubwa, lakini kwa rehema za Mungu pamoja na juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama, mtoto huyo amerejea salama.
Akizungumza kwa hisia kali za shukrani, mama huyo alimshukuru Mungu kwa ulinzi wake katika kipindi chote cha sintofahamu. Alisema kuwa ni neema ya Mungu mtoto wake kupatikana bila madhara yoyote, licha ya mazingira magumu yaliyokuwepo.
“Sifa na utukufu ni kwa Mungu aonaye vya sirini bila yeye, jambo hili lisingewezekana,” alisema kwa sauti ya furaha na shukrani.
Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa Jeshi la Polisi, hususan Jeshi la Polisi Tanzania kupitia kituo cha wilaya ya Kigamboni, kwa juhudi kubwa walizozifanya kuhakikisha mtoto anapatikana pamoja na Matukio Daima Media .
Kwa mujibu wa maelezo yake, askari wa jeshi hilo walifanya kazi usiku na mchana, wakifuatilia kwa karibu kila taarifa iliyoweza kusaidia kumpata mtoto huyo.
Mama huyo alieleza kuwa askari hao walilala barabarani usiku kucha wakimsaka mtuhumiwa, na hatimaye walifanikiwa kumkamata pamoja na kuhakikisha mtoto anarejeshwa kwa familia yake salama.
Alisema kuwa kazi hiyo ni ya kupongezwa na kwamba Mungu atawalipa kwa jitihada zao za kulinda usalama wa raia.
Katika maelezo yake, ilibainika kuwa mtoto huyo alitoroshwa na binti wa kazi wa nyumbani, jambo lililozua mshangao mkubwa kwa familia na majirani.
Mtuhumiwa huyo tayari amekamatwa na anashikiliwa na vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu uangalizi na umakini unaopaswa kuchukuliwa wakati wa kuajiri wafanyakazi wa majumbani.
Mama wa mtoto alitoa rai kwa wazazi na walezi kuwa makini wanapochagua mabinti wa kazi.
Alisema kuwa muhimu kufanya uchunguzi wa kina kuhusu historia na mienendo ya mtu kabla ya kumpa jukumu la kulea watoto au kusimamia nyumba. “Tujifunze kutokana na tukio hili. Tusichukulie mambo kwa wepesi, hasa linapokuja suala la usalama wa watoto wetu,” alionya.
Jamii imetakiwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa mapema pale wanapobaini viashiria vya vitendo vya uhalifu Ushirikiano huo, kwa mujibu wa mama huyo, ndio uliosaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kupatikana kwa mtoto wake.
Kwa sasa, familia inaendelea na taratibu za kumrejesha mtoto katika hali ya kawaida ya maisha huku wakimshukuru Mungu kwa kumlinda.
Tukio hili limeacha somo muhimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa tahadhari, umakini na ushirikiano katika kulinda usalama wa watoto.
USIKOSE KUFUATILIA MAHOJIANO KAMILI KUPITIA CHANEL YA MDTVYETU KESHO ASUBUHI
%20(1).jpg)

.jpg)