KANISA LATOA NG'OMBE SERIKALINI KUCHOCHEA MAENDELEO
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania, Kanisa la Ebenezer Assemblies of God Afrika (EAGA) lenye makao yake makuu mkoani Mbeya, limetoa ng'ombe mwenye thamani ya shilingi laki tano kwa uongozi wa Serikali kata ya Nsalala mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya ili kusaidia kuchochea maendeleo ikiwemo uboreshaji miundombinu ya elimu na barabara.
Zawadi hiyo imetolewa na kanisa la Ebenezer (EAGA) lililopo Mbalizi Mbeya, ambapo waumini wa kanisa hilo wamesema sio mara ya kwanza kushiriki moja kwa moja shughuli za maendeleo ya wananchi.
Akizungumza kwenye ibada iliyofanyika jumapili iliyopita (Februari 22, 2026), Askofu mkuu wa Kanisa la EAGA Mchungaji Peter Hasunga, amesema kanisa la YESU (Ebenezer Mbalizi) limeendelea kuwa mdau wa Serikali kwa muda mrefu kwani hapo awali walikarabati chumba cha darasa katika moja ya shule mjini Mbalizi na kujitoa kujenga kivuko cha wananchi.
Amesema kwa sasa wameamua kutoa ng'ombe na kuikabidhi Serikali ya kata ya Nsalala ili waone mahali penye uhitaji wa kuongeza nguvu hata kuboresha mazingira na miundombinu ya utoaji huduma kwa jamii.
Mch. Hasunga amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuwatumikia wananchi hivyo ni wajibu wa kila mwananchi na taasisi mbalimbali kuiunga mkono Serikali yao ili kufikia maendeleo endelevu.
Akitoa neno la shukrani ibadani hapo, Diwani wa kata ya Nsalala Mhe. Festo Mbilike, amelishukuru Kanisa la Ebenezer (EAGA) linaongozwa na askofu Hasunga kwa maongozi ya Roho Mtakatifu akisema wamehubiri kwa matendo kutoa sadaka yao kwa Serikali ili kusaidia kuchochea shughuli za maendeleo.
Diwani Festo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na kanisa hilo katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika Kanisa na Taifa kwa ujumla ambapo Mhe. Diwani huyo aliambatana na afisa mtendaji wa kata ya Nsalala Bwana Waziri Juma Shunda na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata hiyo Ndg. Michael Ngalya.



