DC SHAKA AHIMIZA USHIRIKIANO
Na Matukio Daima, Kilosa
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wananchi, viongozi wa maeneo na wadau wa maendeleo kushirikiana kwa karibu ili kukamilisha ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Lumuma, wilayani humo.
Wito huo umetolewa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo, ambapo alibainisha kuwa kukamilika kwa mochwari kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha wanazopata wananchi wakati wa misiba.
DC Shaka amesema huduma za afya haziishii kwenye matibabu pekee, bali zinapaswa kugusa mahitaji yote muhimu ya jamii, ikiwemo huduma za kuhifadhi miili ya marehemu kwa heshima na usalama.
“Tusipojipanga kwa pamoja, changamoto hii itaendelea. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya afya,” amesema.
Katika kuonyesha mfano wa uongozi na uwajibikaji, DC Shaka alitangaza kuchangia shilingi milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa chumba hicho, hatua aliyosema inalenga kuhamasisha wadau wengine kujitokeza.
Wananchi wa Kata ya Lumuma wamesema wanatarajia wito huo kuleta matokeo chanya, wakieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakisafirisha miili ya wapendwa wao hadi maeneo ya mbali.
Bi. Avelina William amesema kukamilika kwa mochwari kutapunguza mzigo wa kifedha na kisaikolojia kwa familia zinazopata misiba.
“Tutakuwa tunahifadhi miili hapa hapa, badala ya kukimbia mbali kutafuta huduma,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Lunenzi, Elidad Elias, amesema ushirikiano wa wananchi na Serikali ndio msingi wa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Lumuma, Hassan Mtolilo, amesema uwepo wa mochwari utaboresha mazingira ya kazi na kuongeza ubora wa huduma kwa jamii.
DC Shaka ameahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo pamoja na changamoto nyingine ikiwemo upatikanaji wa maji katika kituo hicho, ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.

