Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DC MNZAVA MGUU KWA MGUU KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

DC MNZAVA MGUU KWA MGUU KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI


Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Mnzava, amefanya ziara maalum katika kata za Mwika Kusini na Marangu Magharibi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kusogeza huduma karibu na jamii.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mnzava aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, hali iliyoonesha dhamira ya Serikali kushughulikia changamoto za wananchi kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali.

Taasisi muhimu za umma zikiwemo RUWASA, MUWSA, TANESCO, KINAPA na TARURA zilishiriki kikamilifu kwenye mikutano ya hadhara, zikitoa ufafanuzi wa papo kwa papo na kueleza mipango ya kutatua changamoto zilizowasilishwa na wananchi.

Changamoto zilizotawala katika mikutano hiyo zilihusu zaidi sekta za maji, barabara, umeme, elimu, afya, mawasiliano, pamoja na masuala ya ulinzi na usalama. Wananchi walieleza adha wanazokutana nazo katika upatikanaji wa maji safi, ubovu wa barabara za vijijini, na changamoto za huduma za kijamii katika baadhi ya maeneo.


Mbali na masuala ya miundombinu, wananchi pia walieleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya ulevi uliopitiliza na matumizi ya dawa za kulevya, hasa miongoni mwa vijana, hali inayotishia ustawi wa jamii.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mhe. Mnzava alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kutatua changamoto hizo.

“Lengo la ziara hizi ni kuwasikiliza wananchi moja kwa moja na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa majibu kwa vitendo. Serikali ipo pamoja na wananchi, na kila taasisi iliyopo hapa ina wajibu wa kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaostahili,” alisema Mhe. Mnzava.

Aidha, alitoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya dola, wazazi, na viongozi wa dini katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vinavyohatarisha maadili ya jamii.

Ziara hiyo imeongeza matumaini kwa wakazi wa Mwika Kusini na Marangu Magharibi, wakiamini kuwa mwitikio wa viongozi na ushirikishwaji wa taasisi mbalimbali utasaidia kuharakisha utatuzi wa kero zao na kuimarisha maendeleo ya maeneo yao.




 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3