BOT : VIKAO NA WAANDISHI WA HABARI VIMELETA MAFANIKIO KWA BENKI
Feb 26, 2026
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
BENKI kuu ya Tanzania imesema kuwa vikao na mikutano inayofanyika baina ya watendaji na wataalam wa benki hiyo na waandishi wa habari imekuwa na tija kubwa kufikishwa kwa taarifa mbalimbali za utendaji wa benki hiyo kwa wananchi.
Meneja Msaidizi idara ya mawasiliano serikalini Benki kuu ya Tanzania, Noves Moses alisema hayo katika mkutano wa siku mbili na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kagera, katavi, Tabora na Kigoma unaofanyika mjini Kigoma ukilenga kuelekeza utendaji na mabadiliko mbalimbali ya utendaji wa benki hiyo.
Meneja huyo alisema kuwa vikao na mikutano hiyo imejenga uelewa mkubwa kwa waandishi wa habari kuhusu shughuli za benki hiyo jambo ambalo limewafanya kutumia taarifa na takwimu mbalimbali zinazotolewa na benki kuandika habari, Makala na kuandaa vipindi kwa ajili ya kuifahamisha jamii kuhusu shughuli za uchumi na biashara.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Mwenyekiti wa Waandishi wa habari katika mkutano huo, Prosper Kwigize alipongeza Benki Kuu ya Tanzania kuandaa mikutano hiyo kwani imesaidia kujenga uelewa mpana kwa waandishi kutumia taarifa na takwimu za benki hiyo katika kufanya kazi zao.
Akitoa mada ya majukumu ya BOT kuhusiana na shughuli na uchumi na biashara Meneja Msaidizi uchumi na biashara wa benki hiyo, Chamy Chamicha alisema kuwa benki kuu kwa sasa imekuwa kwenye uhamasishaji jamii kufanya matumizi kwa kutumia mifumo ya kidijitali badala ya fedha taslim na kwamba waandishi wa habari na vyombo vya habari vimekuwa na mchangp mkubwa kupeleka taarifa hizo kwa jamii.




