WENYE ULEMAVU IRINGA WAPONGEZA NSSF KWA MAFUNZO YA WASTAAFU WATARAJIWA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Watu wenye ulemavu mkoani Iringa wamepongeza Mafunzo ya wastaafu watarajiwa yaliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakisema yamewajengea uelewa mpana kuhusu hifadhi ya jamii na umuhimu wa kujiandaa mapema kwa maisha baada ya ajira.
Wakizungumza na Matukio Daima Media, washiriki hao wamesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu haki zao za msingi katika mifumo ya hifadhi ya jamii, huku wakisisitiza umuhimu wa watu wenye ulemavu kupewa fursa sawa za ajira na kujiunga na NSSF kama ilivyo kwa waajiriwa wengine.
Wamesema kuwa katika taasisi na mashirika mbalimbali nchini wapo watu wengi wenye ulemavu wanaofanya kazi, hususan kwenye sekta binafsi, lakini bado baadhi yao hawajashirikishwa kikamilifu katika mifumo ya hifadhi ya jamii, jambo linalowanyima haki zao za msingi ikiwemo mafao ya uzeeni.
Akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu, Sofian Jafary Kavenuke amesema ni wajibu wa waajiri kuhakikisha wafanyakazi wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanasajiliwa na kuchangiwa michango ya NSSF kwa mujibu wa sheria.
“Kwa mashirika ambayo yameajiri watu wenye ulemavu, ni muhimu kuwapa nafasi ya kujiunga na NSSF. Watu wenye ulemavu wanaofanya kazi kwenye mashirika binafsi wapo wengi, hivyo wanapaswa kushirikishwa ili nao wanufaike na mpango wa NSSF kama wafanyakazi wengine,” amesema Kavenuke.
Aidha, ameiomba NSSF kuendelea kuwafikia watu wenye ulemavu kupitia semina na programu mbalimbali za elimu, ili kuongeza uelewa wao kuhusu hifadhi ya jamii na maandalizi ya maisha baada ya ajira.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amewataka waajiri wote nchini kuhakikisha wanawasilisha michango ya waajiriwa wao kwa NSSF kwa wakati, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni wajibu wa kisheria.
Meya Ngwada ametoa wito huo baada ya kuhudhuria ufunguzi wa semina ya NSSF mkoani Iringa, akibainisha kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa waajiri au taasisi zitakazokiuka sheria.
Hata hivyo, amewahimiza wafanyakazi na wanajamii kwa ujumla kutoiona kustaafu kama tatizo, bali kama hatua ya kawaida ya maisha inayohitaji maandalizi ya mapema ili kuepuka changamoto za kiuchumi na kijamii baada ya kumaliza ajira.



