WAZIRI MKUU AZINDUA MELI YA MV NEW MWANZA, AIPONGEZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameizindua rasmi meli ya kisasa ya MV New Mwanza iliyogharimu takribani kiasi Cha Sh, Bil 120 na kueleza kuwa ni kielelezo cha utekelezaji wa ahadi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Januari 23, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa meli hiyo uliyofanyika Bandari ya Mwanza Kusini na kueleza kuwa meli hiyo imefungua ukurasa mpya wa matumaini, faraja na maendeleo kwa Watanzania, hususani wakazi wa Kanda ya Ziwa, kutokana na uwezo wake mkubwa na viwango vya kimataifa ilivyojengwa.
Dkt, Mwigulu ameeleza kuwa MV New Mwanza ni meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria na ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa matatu.
"Meli hii imepunguza muda wa safari kati ya Mwanza na Bukoba kutoka saa nane hadi saa sita, huku masuala ya usalama yakizingatiwa kikamilifu" Alisema Mwigulu.
Aidha ameipongeza Wizara ya Uchukuzi, Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) pamoja na kampuni zilizoshiriki katika ujenzi wa meli hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ujuzi uliopatikana na kuutumia katika miradi mingine ya ujenzi wa meli, ikiwemo mradi unaoendelea katika Ziwa Tanganyika.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa meli hiyo umetumia gharama ya Dola za Kimarekani 51,830,440.28 sawa na Shilingi 120,562,787,135.31, na ulitekelezwa na kampuni za GAS ENTEC CO. LTD na KANGNAM kutoka Korea Kusini kwa kushirikiana na SUMA JKT.
Mbarawa ameeleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2019 na ulikuwa umefikia asilimia 40 wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, lakini ulikamilika kutokana na uwezeshaji wa kifedha kutoka Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya meli Tanzania TASHICO, Eric Hamiss, amesema meli hiyo ilikamilika Oktoba 2025, na kufanyiwa majaribio pamoja na kukaguliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri kwa Njia ya Maji (TASAC) na kupewa cheti cha ubora.
"Tayari imefanya safari sita kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo, ikihudumia abiria 7,028 na kusafirisha tani 673 za mizigo" Alisema Hamiss.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda alisema uzinduzi wa meli hiyo ni hatua kubwa katika kuboresha usafiri wa majini, kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
Uzinduzi wa MV New Mwanza unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha usafiri wa majini, kukuza uchumi wa kikanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.





