SERIKALI YATOA VIFAA VYA KIDIJITI BILIONI 5.4 KUWAWEZESHA WALIMU WENYE ULEMAVU
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imenunua na kusambaza vifaa vya kidijiti na saidizi vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.4 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi pamoja na walimu tarajali wenye ulemavu katika vyuo vya ualimu nchini, kwa lengo la kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji jumuishi.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 31, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejizatiti kuhakikisha wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalum hawatengeki katika mfumo wa elimu.
Prof. Mkenda amesema jumla ya wanufaika 1,055 kutoka Halmashauri 104 nchini wamenufaika na mpango huo, ambapo vifaa vilivyosambazwa ni pamoja na kompyuta mpakato 680, vifaa tisa vya Brain Note Touch Pass, vinasa sauti (voice recorders) 377, tablet 196 kwa wanaotumia lugha ya alama, mashine 30 za Perkins Braille, vifaa 101 vya kusaidia kusikia pamoja na mashine za Everest Drill Embosser.
Ameeleza kuwa mashine hizo zinawezesha walimu wasioona kuchapa maandishi kwa kutumia nukta nundu (Braille) na baadaye kuchapisha maandishi ya kawaida yanayoweza kusomwa na wanafunzi wengine, hivyo kuimarisha ushiriki sawa katika ufundishaji.
Aidha, amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa vifaa saidizi na vitabu maalum kila mwaka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, huku Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ikihakikisha vitabu vinachapishwa kwa maandishi makubwa kwa wenye uoni hafifu na kwa nukta nundu kwa wasioona kabisa.
Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa ahadi za Rais Samia unaenda sambamba na upanuzi wa fursa za elimu ya juu kupitia mikopo na ujenzi wa miundombinu, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kujenga kampasi mpya 16 za vyuo vikuu katika mikoa ambayo awali haikuwa na kampasi hizo.
Amesema mikoa yote nchini tayari ina vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, huku ujenzi wa kampasi mpya ukiendelea katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Lindi, ikiwemo kampasi za Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwisho

