Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YATOA MIKOPO SH MILIONI 820 AJIRA 546 ZAZALISHWA KWA VIJANA

SERIKALI YATOA MIKOPO SH MILIONI 820 AJIRA 546 ZAZALISHWA KWA VIJANA



Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema serikali kupitia wizara yake imetoa mikopo 193 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 820, hatua iliyosaidia kuzalisha ajira 546, nyingi zikiwa ni kwa vijana.

Waziri Kapinga ameyasema hayo leo Januari 24, 2026, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa siku 100 za Ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya viwanda na biashara.

Amesema katika kipindi hicho, maelfu ya kampuni, majina ya biashara pamoja na leseni za viwanda zinazomilikiwa na vijana zimesajiliwa ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.

Aidha, uanzishwaji wa mitaa ya viwanda na kongani za viwanda umeendelea kuleta matokeo chanya kwa kuzalisha maelfu ya ajira, sambamba na kuandaliwa kwa programu ya kukuza biashara 100,000 zinazomilikiwa na vijana nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema zaidi ya vijana 1,200 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, huku mamia yao wakiunganishwa na programu za uatamizi wa biashara kwa lengo la kuwawezesha kukua kibiashara.

Ameongeza kuwa wafanyabiashara zaidi ya 26,000 wamepata taarifa za masoko kupitia mifumo ya kidigitali, hatua inayochochea ushindani na upanuzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa uzalishaji, amesema serikali inaendelea kuweka kwenye mstari wa uzalishaji viwanda vipya vya nishati mbadala, uchakataji wa mazao, dawa na mbolea, kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi wa viwanda.

"Katika sekta ya kilimo,  wakulima wa korosho wameingiziwa zaidi ya Shilingi trilioni moja moja kwa moja kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, hatua iliyoongeza kipato na uwazi katika mauzo ya zao hilo, " Amesema Waziri Kapinga.

Vilevile, utekelezaji wa miradi ya mpira Kalunga, mkaa mbadala pamoja na tafiti za madini adimu umeelezwa kuimarisha msingi wa uchumi wa kijani na uchumi wa kimkakati, unaolenga maendeleo endelevu ya taifa.


 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3