RC MAKAME ATAKA UAMINIFU VYAMA VYA USHIRIKA SONGWE
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amevitaka vyama vya ushirika mkoani humo kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na uwajibikaji ili kujenga na kuimarisha ushirika imara unaowanufaisha wanachama wake.
Makame ametoa wito huo Januari 30, 2026, mara baada ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa hisa kwa vyama wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (SORECU), pamoja na kuzindua na kukabidhi kwa wanachama gari jipya lililonunuliwa kwa gharama ya shilingi milioni 107.8.
Akiwahutubia viongozi wa vyama wanachama wa SORECU, Makame alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondoa changamoto na malalamiko yanayotolewa na wakulima, ambao ndio wanachama wa msingi wa vyama hivyo.
“Pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa, niwaombe sana kuimarisha uaminifu katika vyama vyetu vya ushirika, kwani bado kumekuwepo na changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakizilalamikia kutokana na utendaji wa baadhi ya viongozi,” alisisitiza Makame.
Aliongeza kuwa serikali, kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika, imefanya mageuzi makubwa ya kiutawala, kiutendaji na kimfumo kuanzia ngazi ya vyama vikuu hadi vyama vya msingi, kwa lengo la kuongeza tija na kuhakikisha ushirika unachangia kikamilifu ukuaji wa sekta ya kilimo na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Meneja Shughuli wa SORECU, Moni Mwampamba, alisema jumla ya vyama vya ushirika 30 vimetunukiwa vyeti vya umiliki wa hisa kati ya vyama 263 vya ushirika vya kilimo na masoko vilivyosajiliwa mkoani Songwe.
Alisema vyama hivyo vinajihusisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara ikiwemo kahawa, ufuta, tumbaku, mahindi, maharage na mpunga.
Akizungumzia gari lililonunuliwa aina ya Ford Ranger Double Cabin lenye thamani ya shilingi milioni 107.8, Mwampamba alisema ununuzi huo ni utekelezaji wa azimio la Mkutano Mkuu wa mwaka 2025, na kwamba gari hilo litasaidia kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za vyama na kuwafikia wanachama kwa haraka zaidi.



