RAIS SAMIA ATOA ZAWADI MAZINYUNGU, WATOTO WAKATA KEKI KUMUUNGA MKONO
Na Matukio Daima,Kilosa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kugusa maisha ya makundi yenye uhitaji maalum baada ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mazinyungu, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa Januari 27, 2026.
Zawadi hizo zilikabidhiwa kwa niaba ya Rais Samia na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, na zilijumuisha magodoro, mashuka, vyandarua, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi pamoja na chakula.
Tukio hilo la kihistoria limefanyika katika kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia, aliyezaliwa tarehe 27 Januari 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Katika tukio hilo lililojaa hisia na tabasamu, wanafunzi wenye uhitaji maalum walikata keki kama ishara ya kuungana na Rais Samia katika siku yake ya kuzaliwa, wakionesha upendo na mshikamano kwa kiongozi wao.


