MHANDISI MARYPRISCA MAHUNDI AMERIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI WA JENGO LA UTAWALA TICD TENGERU.
Jan 23, 2026
Na,Jusline Marco ;Arusha
Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Wizara hiyo ipo kimkakati kuhakikisha mafunzo na huduma katika vyuo vya maendeleo ya Jamii nchini vinaendelea kuboreshwa kwa lengo la kutoa wataalam mahiri watakaoendeleza jamii kupata Ustawi na kuchangia maendeleo katika Taifa.
Mhandisi Mahundi amesema hayo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru TICD,ambapo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amedhamiria kuchangia katika Kila Idara kuhakikisha watumishi na wanafunzi wote wananufaika.
Aidha ameipongeza Taasisi hiyo kwa ubunifu na Usimamizi thabiti wa miradi ya ujenzi na utekelezaji ya majukumu yake hatua inayoendelea kukiweka chuo katika nafasi ya kitaifa kwenye utoaji wa taaluma ambapo ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru TICD katika kuboresha mazingira ya kujifunza na maeneo ya mkifanyia kazi watumishi ambapo ameeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ni nguzo muhimu ya Maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Bakari George ameishukuru serikali kuu kwa utoaji wa fedha za kuendeleza miradi mbalimbali katika Taasisi hiyo na kusema kuwa uwepo wa miradi ya kimkakati katika Taasisi hiyo kunaimarisha utoaji wa taaluma na kuongeza idadi ya wanafunzi.
Akizungumza kwa niaba ya katibu wa chama cha mapinduzi Mkoa, katibu umoja wa wazazi CCM Mkoa ,Ally Jacob Mamelela ameipongeza Taasisi hiyo kwa kufanya jengo la utawaka linalojengwa kuendana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa ambapo pia ametoa pongezi kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha katika kuwezesha miradi mbalimbali nchini inatekelezwa.
Ziara ya Naibu Waziri huyo imeenda sambamba na utembeleaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa utekelezaji wa shughuli za kituo cha kitaifa cha utafiti na uhifadhi wa machapisho yahusuyo wanawake, utekelezaji wa shughuli za kituo cha Huduma tandaa na ubunifu wa kidijitali pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la utawala.




