MCHENGERWA: MAFANIKIO YA BIMA YA AFYA YAPIMWA NA WANANCHI
WAZIRI wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW) hautapimwa kwa idadi ya matamko au maandiko ya sera, bali kwa namna wananchi wanavyopata huduma za afya katika vituo vilivyopo karibu nao.
Ameyasema hayo leo Januari 23,2026 wakati wa kikao kazi cha viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kilichojadili maandalizi ya uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mpango huo, akieleza kuwa afya ni eneo la msingi katika maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali imeamua kuanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ili kuimarisha mifumo ya usajili, utoaji huduma na usimamizi wa bima kabla ya kuwahusisha wananchi wote.
"Awamu ya kwanza italenga wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama za bima yao zitagharamiwa na Serikali, " Amesema Waziri huyo
Aidha ameeleza kuwa Wakuu wa Mikoa wanabeba dhamana ya moja kwa moja ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao, huku mafanikio ya kila Mkoa yakitarajiwa kuakisi kiwango cha uongozi na ufuatiliaji.
Amesema kuwa viongozi wa Wilaya na Halmashauri wanapaswa kuhakikisha usajili wa wananchi unafanyika hadi ngazi ya kata, kijiji na mtaa ili kuondoa mianya ya mwananchi kubaki nje ya mfumo wa bima.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha mfumo mmoja wa kitaifa wa kidijitali wa afya utakaounganisha huduma, usimamizi wa bima na udhibiti wa gharama.
" Ubora wa huduma katika vituo vya afya ni kichocheo muhimu cha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisisitiza kuwa huduma kwa mwananchi ni haki na si hisani, " Amesema Waziri Mchengerwa.





