MAUWASA yaonya wezi wa Maji
Jan 26, 2026
Sehemu ya jengo la Ofisi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA).
Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
Mamlayka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) imewaonya wananchi wanaojiunganishia huduma ya maji kinyume cha sheria kuacha mara moja vitendo hivyo, ikisema hatua hizo zinasababisha hasara kubwa kwa mamlaka hiyo na kuhatarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi wengine.
Akizungumzia suala hilo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias alisema kuwa wamebaini kuwepo kwa baadhi ya wananchi wanaojiunganishia maji bila kufuata taratibu za kisheria, jambo linalochangia matumizi ya maji bila malipo pamoja na uharibifu wa miundombinu ya maji.
Alisema kuwa vitendo vya kuingilia miundombinu ya maji siyo tu vinakiuka sheria ya maji ya mwaka 2019, bali pia vinaweza kusababisha usumbufu wa huduma kwa wananchi wanaolipa kwa uhalali.
“Tumebaini kuwa baadhi ya watu wanaharibu na kuingilia miundombinu ya Mauwasa kwa kujipatia maji kinyume cha sheria. Hili ni kosa kubwa na linasababisha hasara kwa mamlaka ya umma pamoja na kuathiri upatikanaji wa maji kwa wananchi wengine,” alisema.
Alitolea mfano wa tukio la januari 23,2026 ambapo Mauwasa ilimkamata mwananchi aitwaye Esther Daud, mkazi wa Uzunguni mjini Maswa, akitumia maji ambayo hayakuwa yakipitia kwenye mita kwa kipindi cha miezi minne.
“Esther Daud alikuwa anatumia akaunti ya maji ya Ladislaus Kiatu, mkazi wa Uzunguni. Huduma yake ilisimamishwa kutokana na kushindwa kulipa bili ya maji, lakini tumemkamata akijiunganishia maji kinyume cha sheria. Tayari tumemkabidhi kwa vyombo vya sheria ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema.
Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa watumiaji wote wa huduma zake kama sehemu ya jitihada za kudhibiti wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu.
MAUWASA imewataka wananchi wote wanaohitaji huduma ya maji kufuata taratibu rasmi za kuunganishiwa huduma hiyo, huku ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujiunganishia maji kinyume cha sheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uzunguni mjini Maswa, Caroline Shayo, alilaani vikali vitendo vya wizi wa maji amesema kuwa ni sawa na uhujumu wa uchumi na vinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya jamii.
“Nilishuhudia tukio hilo na ni kweli kabisa. Wizi wa maji ni sawa na kuhujumu mali ya umma. Maji ni rasilimali ya wote, hivyo yeyote anayeyaiba anawanyima wengine haki yao,” alisema.
Naye Getruda John mkazi wa mjini Maswa alisema kuwa anaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Mauwasa huku akitaka sheria isimamiwe bila muhali.
“Tunaojiunganishia kihalali tunapata shida kubwa. Maji yanapungua au kukatika kwa sababu kuna watu wanajiunganishia kwa siri,” alisema.
Bomba la maji linaloingiza maji katika nyumba ya Esther Daud mkazi wa uzunguni mjini Maswa.maji ambayo ambayo hayapiti kwenye mita na mtumiaji kutumia bila kuyalipia.
MWISHO.


