GARI ZILIZOTAIFISHWA NA TRA ZAKABIDHIWA MAGEREZA, ZIMAMOTO
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) imekabidhi kwa jeshi la magereza na jeshi la zimamoto mkoa Kigoma magari mawili yaliyotaifishwa na mamlaka hiyo kwa kuingizwa nchini kwa njia ya magendo bila kulipiwa ushuru.
Meneja wa TRA mkoa Kigoma, Beatus Nchota kwa niba ya Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo alikabidhi Magari hayo ambapo kwa Mkuu wa wilaya za Kigoma, Rashid Chuachua alikabidhi roli aina ya Fuso ambalo limekabidhiwa kwa jeshi la Magereza na kwa Mkuu wa wilaya Buhigwe,Kanali Michael Ngayarina alikabidhiwa gari aina ya Toyota Alphard kwa niaba ya jeshi la zimamoto wilaya Buhigwe.
Akizungumza kabla kukabidhi magari hayo Meneja wa TRA mkoa Kigoma, Beatus Nchota alisema kuwa lengo la Mamlaka hiyo kukabidhi magari hayo ni kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kutatua changamoto ya upungufu wa usafiri katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Buhigwe, Kanali Michael Ngayarina ameishukuru TRA kwa kuona na kuthamini mchango wa taasisi hizo za ulinzi na usalama kwani magari hayo yangeweza kwenda taasisi nyingine za serikali lakini wameona mchango wa taasisi hizo katika suala la ulinzi na usalama wa mkoa Kigoma.
Akizungumza baada ya kupokea gari aina ya Fuso kutoka kwa mkuu wa wilaya Kigoma, Kamishna Msaidizi wa Magereza ambaye ni Mkuu wa magereza mkoa Kigoma, Mussa Mkisi kwa niaba ya Mkuu wa jeshi la magereza nchini alisema kuwa kuwa gari hilo ni msaada mkubwa kwao katika kusaidia usafirishaji wa mazao kutoka kwenye mashamba ya jeshi hilo yaliyopo kwenye wilaya mbalimbali za mkoa huo sambamba na kusafirisha wafungwa kwenda kwenye maeneo ya uzalishaji na shughuli mbalimbali.


