TNCC YAONYA UTAPELI KUDHOOFISHA BIASHARA KIGOMA NA DRC
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
CHEMBA ya Taifa ya biashara (TNCC) mkoani Kigoma imewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kuimarisha uaminifu na uadilifu katika kufanya biashara na wafanyabiashara wenzao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Meneja wa TNCC Mkoa wa Kigoma, Prosper Guga, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, akieleza kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara kutoka DRC kuhusu kutapeliwa na wenzao wa Kigoma akieleza kuwa yanaweza kuathiri ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.
Alisema ni muhimu wafanyabiashara kuzingatia maadili, uaminifu na kutimiza makubaliano wanayoingia na wenzao kwa kuwa biashara ya kuvuka mpaka inategemea zaidi kujenga mahusiano ya muda mrefu na kuaminiana ambapo alisema kuwa TNCC imeingia makubaliano na Chemba ya biashara ya DRC kusaidia kukuza biashara na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo.
Akieleza hali hiyo alisema kuwa TNCC imeanza kulipatia ufumbuzi suala la Mfanyabiashara wa DRC na wenzake waliotapeliwa milioni Zaidi ya 90 mwaka 2024 ambapo katika kulifuatilia jambo hilo tayari mfanyabiashara huyo wa Kigoma ameanza kulipa deni hilo kwa juzi kutoa kiasi cha milioni 20.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mmoja kutoka DRC,Anne Shilwalwa Maombi alisema alikuwa anashirikiana na Mfanyabiashara mmoja waa Kigoma ambaye alikuwa akimletea unga wa ngano kutoka Dar es Salaam kuleta Kigoma na yeye kupeleka DRC ambapo baadaye alimuamini na kumpatia kiasi cha milioni 90 mwaka 2024 kuwa wakala wao lakini mfanyabiashaara huyo alitumia fedha hizo kwa manufaa yake badala ya kutekeleza makubaliano hali iliyosababisha usumbufu mkubwa na kuyumbisha shughuli zao za biashara.
Maombi alisema kuwa tangu mwaka 2024 amehangaika maeneo mbalimbali ikiwemo polisi lakini hakupata mafanikio hadi mwezi uliopita alipoenda ofisi za TNCC ambapo baada ya kueleza changamoto yake ilifanyiwa kazi na wiki hii amepatiwa kiasi cha shilingi milioni 20 ikiwa sehemu ya fedha alizokuwa ametapeliwa.
Kutokana na hilo Mfanyabiashara huyo aliishukuru TNCC kwa kuingilia kati na kusimamia suala hilo, akisema kuwa hatua hiyo imeanza kuleta matumaini ya taasisi hiyo katika kusimamia changamoto za wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.
Mwisho.


