45 WANOLEWA KUSIMAMIA UCHAGUZI MDOGO KATA YA LUGENGE NJOMBE
Serikali kupitia Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania imewataka wasimamizi wa Uchaguzi mdogo kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa pasina kuwa kikwazo kwa mawakala wa vyama vya siasa na wapiga kura wakati wa uchaguzi.
Katika mkoa wa Njombe kata moja ya Lugenge Halmashauri ya mji wa Njombe ndiyo itakayohusika katika uchaguzi wa diwani ikiwa jumla ya Wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi 45 pamoja na wawili wa ziada kwenye vituo 15 vya kupigia kura wameanza mafunzo ya siku mbili Kwa ajili ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika hapo Novemba 4 mwaka huu.
Akifungua mafunzo hayo Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Njombe Mjini Gabriel Kulaba amewataka wasimamizi hao kutambua kuwa hakuna atakayeachwa salama endapo atakiuka sheria na kanuni za uchaguzi ikiwemo kutunza siri.
Lewis Mnyambwa ni mratibu wa uchaguzi mkoa wa Njombe ambaye anawaonya wasimamizi hao kujiepusha na ulevi wakati wa uchaguzi pamoja na kuwa nadhifu.
Simon Kilawa na Shemsa Issa ni miongoni mwa wasimamizi 45 walioanza mafunzo hayo ambao wanawaahidi mawakala wa vyama vya siasa na wapiga kura wa kata ya Lugenge kuwa hawatokuwa kikwazo katika uchaguzi huo.
Jumla ya wapiga kura 4833 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo wa kumpata diwani wa kata baada ya aliyekuwepo Philoteus Mligo kufariki ikiwa vyama viwili vya siasa vya CCM na CHAUMA Ndivyo vinavyoshiriki katika zoezi hilo.


