Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TLS YAENDELEA KUMFUATILIA RAIS WAKE, YATOA TAARIFA KWA UMMA

TLS YAENDELEA KUMFUATILIA RAIS WAKE, YATOA TAARIFA KWA UMMA

Na Matukio Daima Media

DAR ES SALAAM

 Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) linaendelea kufuatilia kwa ukaribu shauri la maombi namba 4 la mwaka 2026 lililofunguliwa tarehe 27 Mei 2026 na Wakili Chacha Mwita Nashon, mwenye namba ya uwakili 11554, dhidi ya Rais wa TLS, Wakili Boniface A.K. Mwabukusi, katika Kamati ya Kitaifa ya Maadili ya Mawakili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TLS, shauri hilo limefunguliwa dhidi ya Wakili Mwabukusi kutokana na madai yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu yake kama Rais wa TLS.

Aidha, Baraza la Uongozi limetaja kuwa Oktoba 14, 2026, Rais wa TLS, Wakili Boniface A.K. Mwabukusi, aliitwa na Jeshi la Polisi na kufika Kituo Kikuu cha Polisi Kati, Dar es Salaam, kwa ajili ya mahojiano kuhusu maelezo aliyoyatoa, huku uchunguzi ukiendelea.

Baraza hilo limefafanua kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 4(d) cha Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS Act), Sura ya 307, miongoni mwa majukumu ya TLS ni kuwawakilisha, kuwalinda na kuwasaidia wanachama wake wote.

Limeongeza kuwa litaendelea kumuunga mkono na kumsimamia Rais wa TLS katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea wanachama wa chama hicho, pamoja na kutoa mrejesho wa kina kwa wanachama na umma kuhusu hatua zinazohusiana na shauri hilo.

TLS imewahimiza mawakili wote kuendelea kushikamana, kusimamia haki na kuheshimu utu wa kila wakili nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa TLS, Laetitia Petro Ntagazwa, Oktoba 17, 2026.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3