STAMICO YAPAA KIMAPATO, YALENGA KUINUA WACHIMBAJI WADOGO
Na Matukio DaimaMedia
Mapato ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yameongezeka kutoka Sh bilioni 1.3 mwaka 2018/19 hadi Sh bilioni 149.8 mwaka 2025/26, huku shirika hilo likiimarisha miradi ya uchimbaji, kupanua huduma kwa wachimbaji wadogo na kuweka mikakati ya kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dkt CPA. Venance Mwasse, amesema hayo wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika kikao kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), jijini Dar es Salaam.
Amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa taarifa za kijiolojia, mitaji, elimu ya uchimbaji na teknolojia bora, hali inayoweza kuathiri ufanisi na uzalishaji wao.
Aidha, amesema shirika linaimarisha tafiti za kijiolojia, kuongeza mitambo ya uchimbaji na uchorongaji na kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika shughuli zao.
Sambamba na hilo, katika suala la mitaji, STAMICO inalenga kuwaunganisha wachimbaji wadogo na taasisi za fedha ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo. Mfumo wa dhamana ya mikopo (Credit Guarantee Scheme) umetajwa kuwa mojawapo ya njia zinazoweza kusaidia, ingawa baadhi ya wachimbaji bado wanashindwa kutimiza masharti ya mikopo.
Hata hivyo, shirika hilo pia linataka kuwashirikisha wadau wengine, wakiwemo madalali na wafanyabiashara wa madini, ili kupanua fursa za biashara na kuongeza manufaa ya sekta hiyo kwa wananchi.
Dkt Mwasse amesema Katika kuimarisha uzalishaji, STAMICO inaendelea kuboresha miundombinu ya mradi wa Kiwila, ikiwemo ukarabati wa majengo. Pia ina mikakati ya kuongeza mitambo ya uchorongaji ili kupanua huduma kwa wateja wanaohitaji huduma za utafutaji na uchimbaji wa madini.
Halikadhalika, Dkt CPA Mwasse amesema kwa upande wa viwanda, shirika lina mipango ya kuendeleza shughuli zake Tabora, Singida na Kiwila, pamoja na mtambo wa kutengeneza kokoto uliopo Dodoma. Hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua masoko ya madini na bidhaa zake.
Hata hivyo, amesema katika historia yake, STAMICO ilikabiliwa na changamoto zilizoathiri baadhi ya miradi yake. Mwaka 2020, Serikali ilielekeza mageuzi ya kiutendaji kupitia falsafa ya 4R, iliyolenga maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya mifumo ya utendaji.
Ameongeza kuwa, mageuzi hayo yalilenga kuboresha usimamizi wa miradi na watumishi, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwezo wa shirika kujiendesha kifedha. STAMICO pia imegusia uwezekano wa kuingia katika soko la hisa kama mojawapo ya ajenda zinazoweza kuangaliwa katika kupanua fursa za uwekezaji.
Aidha, amesema kupitia mikakati hiyo, shirika linalenga kuongeza mchango wake katika sekta ya madini na kuwapa wachimbaji wadogo na wadau wengine fursa zaidi za kushiriki katika uzalishaji, uchakataji na biashara ya madini nchini.

