Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DUWASA KUPANDISHA UZALISHAJI MAJI HADI LITA MILIONI 121 KWA SIKU

DUWASA KUPANDISHA UZALISHAJI MAJI HADI LITA MILIONI 121 KWA SIKU


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media  Dodoma

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imepanga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 91 kwa siku hadi lita milioni 121 kupitia mpango mkakati na mpango wa biashara wa miaka mitano unaolenga kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Dodoma.

Hatua hiyo inalenga kupunguza pengo kati ya mahitaji na uzalishaji wa maji, ambapo kwa sasa mahitaji ya maji jijini Dodoma ni lita milioni 159.9 kwa siku, huku uwezo wa mamlaka hiyo kuzalisha maji ukiwa lita milioni 91 kwa siku.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 26, 2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya huduma ya maji safi, utekelezaji wa miradi na uharibifu wa miundombinu ya DUWASA, Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Mhandisi Aron Joseph, amesema uzalishaji wa sasa unakidhi takribani asilimia 57 ya mahitaji ya maji ya jiji hilo.

"Hali hiyo inachangia changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dodoma, huku mahitaji yakitarajiwa kuongezeka hadi kufikia lita milioni 180 kwa siku ifikapo mwaka 2030," Amesema.

Ameeleza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, DUWASA imeandaa mpango wa kuongeza uzalishaji wa maji hadi lita milioni 121 kwa siku, kupitia miradi mbalimbali iliyokwishaandaliwa na mingine iliyoanza kutekelezwa yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 51.

Aidha, amebainisha kuwa DUWASA imepanga kutekeleza mradi wa kuongeza huduma ya maji katika Mji wa Serikali wenye thamani ya Shilingi bilioni 35, utakaohusisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa zaidi ya lita milioni sita, pamoja na ujenzi wa mtandao wa kusafirisha na kusambaza maji wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60.

Amesema mradi huo unalenga kuhudumia Mji wa Serikali na maeneo yanayouzunguka ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Joseph amesema eneo la Makutupora ni chanzo kikuu cha maji kinachoiwezesha DUWASA kuzalisha sehemu kubwa ya maji yanayotumika jijini Dodoma.

Amesema chanzo hicho kinazalisha lita milioni 61.5 za maji kwa siku, huku kiasi kingine kikizalishwa kupitia vyanzo vidogo vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Ametaja baadhi ya vyanzo hivyo kuwa ni Nzuguni, Iyumbu, Nala, Ihumwa, Nkuhungu, Miganga, Mkonze na Makulu, ambavyo vinachangia katika uzalishaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa Dodoma.

Aidha, ameeleza kuwa DUWASA inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyanzo vya maji, hali inayohitaji juhudi za kuongeza uwezo wa uzalishaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa jiji na ongezeko la watu.

Amesema kwa sasa mamlaka hiyo ina visima 72 vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Dodoma, huku visima 17 vilivyopo Makutupora vikichangia sehemu kubwa ya maji yanayozalishwa.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya kuongeza uzalishaji na kuboresha miundombinu ya usambazaji ni sehemu ya juhudi za DUWASA za kupunguza pengo la maji na kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mahitaji ya maji jijini Dodoma bado ni makubwa kuliko kiwango kinachozalishwa kwa siku, jambo linaloifanya mipango ya kuongeza uzalishaji na kuimarisha vyanzo vya maji kuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Mwisho





 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3