Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DIRA 2050: VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UJASIRIAMALI

DIRA 2050: VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UJASIRIAMALI


Na Matukio daima Media MOROGORO

Vijana nchini wametakiwa kutumia ubunifu na ujasiriamali kujitengenezea ajira badala ya kutegemea kuajiriwa, kutokana na ushindani mkubwa katika soko la ajira unaosababisha maelfu ya wahitimu kukosa nafasi za kazi kila mwaka.

Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza katika Mkutano wa 26 wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe uliofanyika Mkoani Morogoro ambapo amewataka wahitimu kuzingatia uadilifu, maadili na kutumia maarifa waliyoyapata chuoni kutatua changamoto za jamii.

Amesema soko la ajira nchini lina ushindani mkubwa kutokana na idadi ya wahitimu wanaoingia kila mwaka, hali inayowalazimu vijana kubadili mtazamo na kuanza kujitengenezea fursa badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Amesisitiza kuwa wahitimu wa fani ya ujasiriamali wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuanzisha biashara na kutengeneza ajira kwa wengine, badala ya kutegemea kuajiriwa katika taasisi kama benki, hospitali na sehemu nyingine za kazi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema mkutano wa baraza la wahitimu ni fursa muhimu kwa chuo hicho kujitathmini na kupokea maoni kutoka kwa wahitimu wake kuhusu ubora wa elimu inayotolewa.

Amesema mrejesho unaotolewa na wahitimu kuhusu uzoefu wao katika maeneo mbalimbali ya kazi unasaidia chuo kubaini mapungufu na kuboresha ufundishaji, tafiti na programu za mafunzo ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

“Tunajikagua na wahitimu wetu wanatupa mrejesho kutoka maeneo mbalimbali wanakofanya kazi, wakitueleza namna wahitimu wetu wanavyotazamwa na waajiri pamoja na jamii,” amesema.

Profesa Mwegoha amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kusimamia falsafa ya kutoa mafunzo yanayozingatia ujuzi, hatua inayolenga kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.

Ameongeza kuwa chuo hicho kimechangia katika kuandaa viongozi mbalimbali nchini, akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye Afisa Habari wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Neemia Mlayo, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, amesema BRELA imeshirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe kuwaandaa wanafunzi kwa kuwapatia elimu itakayowawezesha kutambua na kutumia changamoto zilizopo katika jamii kama fursa za kibiashara baada ya kuhitimu.

Amesema BRELA imeandaa mikakati ya kuwawezesha na kuwahamasisha vijana kurasimisha biashara zao, ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi katika mifumo rasmi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mlayo amesema wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa wanufaika wa elimu hiyo, inayolenga kuwajengea uelewa kuhusu taratibu za usajili wa biashara na umuhimu wa kufanya shughuli za ujasiriamali katika mfumo rasmi.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3