DC LUGANGIRA AWATAKA VIONGOZI WA SETIKALI NGAZI YA MKOA, WILAYA HADI HALMASHAURI KUHAKIKISHA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE UNATEKELEZWA KWA UADILIFU.
Oct 22, 2026
Na,Jusline Marco:Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Neema Lugangira ametoa wito kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Halmashauri, kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoingia mikataba vinakuwa tayari muda wote kutoa huduma kwa wanachama wa Bima ya Afya kwa Wote.
Bi.Lugangira ametoa wito huo wakati akizindua Awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa wote kwa Mkoa wa Arusha,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA. Amosi Makalla, na kusema kuwa utayari wa vituo hivyo unapaswa kujumuisha mifumo ya kuhakiki uanachama, utaratibu wa kutoa rufaa na njia mbadala za kuendeleza huduma pale kunapojitokeza hitilafu za kiufundi, ambapo ameelekeza kila kituo kuwa na utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi pamoja na kuweka wazi taarifa kuhusu mafao, haki na wajibu wa wanachama.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kwa kuwataka viongozi wa Wilaya, halmashauri na wataalamu wa afya kwa ngazi zote Mkoa wa Arusha kuhakikisha Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatekelezwa kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kuwafikia wananchi wote wanaohitaji huduma za afya.
Amesema ni muhimu kwa Viongozi wa ngazi zote kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatafsiriwa katika huduma halisi zinazomfikia mwananchi wa kawaida, wakiwemo wakulima, wafugaji, wafanyabiashara wadogo, waendesha bodaboda, vijana, wazee na wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Amesisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote inalenga kulinda familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu, kupunguza umasikini unaotokana na maradhi na kuhakikisha wananchi hawalazimiki kuuza mali zao au kukopa fedha ili kupata huduma za afya.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila akizungumza katika uzinduzi huo wa Bima za Afya amesema takribani Kaya 7,416 zisizo na uwezo kati ya kaya 12,673 Mkoani Arusha, sawa na asilimia 58.5, zimesajiliwa na kulipiwa gharama za kifurushi cha Bima ya Afya kwa Wote ndani ya siku 100 za awali za Awamu ya Pili ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Nguvila ameeleza kuwa zoezi la kuwasajili na kuwalipia kaya zisizo na uwezo ni endelevu, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kukabiliwa na changamoto za gharama za matibabu.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, huku akieleza kuwa jukumu kubwa lililopo sasa ni kupanua wigo wa usajili na kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho vya bima ili waweze kunufaika na huduma za afya wakati wote.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximiallian Iranghe, akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa Halmashauri za mkoa wa Arusha, ameahidi kushirikiana na viongozi wengine kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa Bima hizo, Mzee Laban Mollel amesema bima hiyo ina manufaa makubwa, hasa kwa kaya maskini ambazo sasa zina uhakika wa kupata huduma bora za afya ambapo ameimshukuru serikali ya awamu ya sita kwa mpango huo na kuwataka Watanzania kujitahidi kuwa na bima ya afya kwa ajili ya kulinda afya na ustawi wa familia zao.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Arusha Bw. Hipoliti Lello amesema kuwa serikali imeweka kipaumbele kwa kaya zisizo na uwezo ambapo kwa Mkoa wamelenga kusajili Kaya 29, 334 zenye jumla ya wanufaika 80, 909 ambazo Kaya hizo zitalipiwa na serikali.




