Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ALAT KUKUTANISHA HALMASHAURI 184 MWANZA, ZAIDI YA WASHIRIKI 500 KUTARAJIWA

ALAT KUKUTANISHA HALMASHAURI 184 MWANZA, ZAIDI YA WASHIRIKI 500 KUTARAJIWA

 


NA CHAUSIKU SAID -MATUKIO DAIMA MWANZA.


Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unatarajiwa kufanyika jijini Mwanza, ukihusisha halmashauri 184 pamoja na wajumbe mbalimbali kutoka maeneo tofauti nchini, wakiwemo mameya.


Mkutano huo, ambao ni miongoni mwa mikutano ya kikanuni ya jumuiya hiyo, unatarajiwa kushirikisha zaidi ya washiriki 500 na kufanyika kuanzia Novemba 14 hadi 26 mwaka huu.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Sima Cosintatine, amesema mkutano huo utakuwa na sehemu mbili, ikiwemo Mkutano Mkuu utakaopitia na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu halmashauri nchini.


Amesema sehemu ya pili itakuwa mkutano wa wadau, utakaokutanisha taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na Serikali za Mitaa, ambazo zitapata fursa ya kuwasilisha mada na kujadili ajenda mbalimbali zinazohusu maendeleo ya Serikali za Mitaa.



Sima amesema maandalizi ya mkutano huo yameanza, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuruhusu na kutoa vibali vya kufanyika kwa mkutano huo.


Aidha, amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kuwa wakarimu kwa wageni watakaofika kushiriki mkutano huo, akieleza kuwa ujio wao ni fursa muhimu ya kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza mzunguko wa fedha katika mkoa huo.


Ameongeza kuwa Mwanza ina vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Kisiwa cha Saa Nane, na kwamba wanaangalia namna bora ya kuwawezesha wageni watakaohudhuria mkutano huo kutembelea vivutio hivyo ili kuitangaza zaidi mikoa na kukuza utalii.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3