WANAWAKE WACHIMBAJI GEITA WATOA WITO: “WANAWAKE JITOSENI KWENYE UCHIMBAJI, NI FURSA YA UCHUMI NA UWEZESHAJI”
Na Matukio Daima Geita
MWENYEKITI wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Mkoa wa Geita (GEWOMA), Asia Masimba, amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi na kujihusisha na shughuli za uchimbaji madini, akisema sekta hiyo ni miongoni mwa fursa muhimu zinazoweza kuwainua kiuchumi, kuongeza heshima na kuimarisha maisha ya familia
Masimba ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita, katika Maonesho ya Tisa ya Madini, yanayofanyika mkoani humo.
Amesema GEWOMA ina zaidi ya wanawake wachimbaji 400 katika Mkoa wa Geita, ambao wamejikita katika shughuli mbalimbali za uchimbaji na sasa wamekuwa mfano wa kuigwa kutokana na hatua kubwa wanazopiga katika kujikwamua kiuchumi.
Kwa mujibu wa Masimba, wanawake hao si tu kwamba wameweza kuongeza kipato chao, bali pia wamekuwa na mchango mkubwa katika kuendesha familia zao na kuboresha maisha ya jamii zinazowazunguka.
“Tunawahamasisha wanawake wajitokeze na kuingia kwenye uchimbaji kwa sababu hii ni kazi yenye fursa kubwa. Wanawake wanaweza kufanya kazi hii na kujenga maisha yao pamoja na kusaidia familia zao,” alisema Masimba.
Aidha, amewataka wanaume kuwaunga mkono wake zao wanaotaka kujihusisha na shughuli za uchimbaji madini, akisisitiza kuwa sekta hiyo inaweza kuwa chanzo muhimu cha kipato na maendeleo ya familia.
Amesema uchimbaji madini si suala la wanaume pekee, bali ni eneo ambalo wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu na kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi wao.
“Tunawaomba wanaume wawaruhusu na kuwaunga mkono wake zao wanaotaka kufanya uchimbaji. Uchimbaji ni maisha, ni fursa na ni utajiri ambao unaweza kubadilisha maisha ya familia,” amesema.
Akizungumzia ushiriki wao katika Maonesho ya Tisa ya Madini, Masimba amesema wanawake hao wamekuja na bidhaa mbalimbali, zikiwemo dhahabu na shaba, huku wakitumia fursa hiyo kujifunza teknolojia mpya zinazotumika katika shughuli za uchimbaji.
Amesema teknolojia hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini, tofauti na zamani ambapo wachimbaji walilazimika kutegemea zaidi nguvu za mikono na uzoefu wa kutafuta maeneo yenye madini.
“Zamani tulikuwa tunatumia zaidi mikono katika kutafuta madini, lakini sasa kuna teknolojia mpya ambazo zinaweza kusaidia kubaini kama eneo lina dhahabu au halina. Hii inatusaidia kufanya uchimbaji kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Amesema wanawake wa GEWOMA wameendelea kujifunza mbinu mbalimbali za uchimbaji, kuanzia kuchimba na kutoa mawe hadi kuyafanyia uchakataji ili kupata dhahabu, huku wakijengewa uwezo wa kutumia zana na teknolojia zinazorahisisha kazi hiyo
Masimba amesema hatua hiyo inaonyesha namna wanawake wanavyoendelea kubadilika na kuingia katika shughuli za uchimbaji kwa ujasiri, maarifa na teknolojia, jambo analodai linaweza kuongeza tija na manufaa ya shughuli za madini kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini, kujenga vikundi imara, kuongeza ujuzi na kutumia teknolojia ili kuongeza thamani ya kazi wanayoifanya.
MWISHO
⬇️⬇️⬇️
MATUKIO DAIMA IMETEULIWA KUSHIRIKI TUZO ZA UMAHIRI WA VYOMBO VYA HABARI NA WANAHABARI TANZANIA TUZO HIZI ZIMETOLEWA NA TCRA NA TAMWA
MAARUFU KWA JINA LA SAMIA KALAMU AWARDS (SKA2026)⬇️⬇️⬇️
1:TUZO YA CHOMBO CHA HABARI -MATUKIO DAIMA MEDIA
PIGA KURA YA CHOMBO MATUKIO DAIMA BONYEZA HAPA
2:TUZO YA JINSIA ,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM
PIGA KURA YA PILI YA MATUKIO DAIMA BONYEZA HAPA
3:TUZO YA AFYA
PIGA KURA YA TATU YA MATUKIO DAIMA BONYEZA HAPA
4:TUZO YA MPIGA PICHA
PIGA KURA YA TATU YA MATUKIO DAIMA BONYEZA HAPA
AHSANTE KWA KUPIGIA KWA KUENDELEA KUTUPIGIA KURA MATUKIO DAIMA MEDIA ENDELEA KUTUPIGIA KURA KILA BAADA YA SAA 24 HADI SEPT 30 KASI YAKO YA KUPIGA KURA NDIO USHINDI .

