HELVETAS YATAKA SERIKALI KUENDELEA KUUNGA MKONO MIRADI YA NISHATI SAFI
Shirika la Helvetas Tanzania limeitaka Serikali kuendelea kuunga mkono uwekezaji katika miradi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira ili kuongeza manufaa kwa jamii na kuhakikisha juhudi za wadau katika eneo hilo zinaendelea.
Mkurugenzi wa Helvetas Tanzania, Daniel Kalimbiya, amesema ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na watoa huduma ni muhimu katika kuhakikisha miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira inaendelea kutekelezwa.
Kalimbiya ametoa kauli hiyo wilayani Ulanga mkoani Morogoro wakati wa hafla ya kufunga na kukabidhi matokeo ya Mradi wa Uwezeshaji Jamii katika Usimamizi Endelevu wa Misitu na Nishati Mbadala, USEMINI uliokuwa ukitekelezwa na Helvetas, Umoja wa Ulaya EU, Mjumita na wadau wengine wa maendeleo.
Naye Msimamizi wa Mradi wa USEMINI kutoka Helvetas Tanzania, Shoma Nangale, amesema miradi hiyo imekuwa nyenzo muhimu kwa vijana kupata fursa za ajira pamoja na kushiriki katika shughuli za uzalishaji zinazoweza kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa viwanda.
Nangale amesema kuendelezwa kwa miradi hiyo kunaweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii huku ikiendelea kuchangia katika uhifadhi wa misitu na mazingira.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba, amesema nishati mbadala sasa ni miongoni mwa maeneo yanayopaswa kupewa msukumo mkubwa katika jamii.
Simba amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwa ajili ya wananchi inakuwa na ufanisi na inatunzwa ili iweze kuendelea kutoa manufaa yaliyokusudiwa.
Aidha amewataka wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri zilizonufaika na miradi hiyo kuhakikisha inatunzwa na kuendelezwa, ili iweze kuendelea kutekeleza malengo ya kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.





