ASKOFU MIHALI AWATAKA WAZAZI KUENDANA NA DIRA 2050 KWA KUWEKEZA KATIKA ELIMU
NA MATUKIO DAIMA MEDIA IRINGA
Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Romanus Elamu Mihali amewataka wazazi na walezi kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto akisema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtoto, familia na taifa kwa ujumla.
Askofu Mihali ametoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule ya St. Dominic Savio, ambapo amesisitiza kuwa elimu ni urithi mkubwa ambao mzazi anaweza kumuachia mtoto wake.
Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu katika kuwaandaa watoto kwa maisha ya baadaye na kuchangia katika ujenzi wa taifa.
“Ili kuendana na Dira yetu ya 2050 inayolenga malezi bora kwa vijana wetu, ningependa kuwasihi wazazi na walezi kuweza kuacha urithi wa elimu kwa watoto wao ili kusaidia kuchochea maendeleo ya Taifa kwa sababu elimu ni maisha.”
Aidha Askofu Mihali amewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika Shule ya St. Dominic Savio alisema shule hiyo inatoa elimu pamoja na malezi yenye kuzingatia maadili.
Alisema mafanikio yaliyooneshwa na wanafunzi katika mahafali hayo, ikiwemo katika elimu, michezo na nidhamu, ni sehemu ya ushahidi wa ubora wa malezi na elimu inayotolewa shuleni hapo.
“Shule za St. Dominic ni shule bora na nzuri sana kwa watoto wetu Kama ambavyo wao wenyewe watakuwa wameshuhudia kwa yale yaliyotolewa kwa muhtasari katika mahafali haya ikiwemo michezo, kauli zao na upande wa elimu inaonesha kuwa katika shule hii elimu inayotolewa ni njema na nzuri.”
Hatahivyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkimbizi A, Aghata Kasisi amepongeza uongozi wa Shule za St. Dominic kwa kutoa elimu bora na malezi yanayojenga nidhamu na kujiamini kwa watoto, akisema shule hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu Manispaa ya Iringa.
“Leo nimeshuhudia mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba wanaomaliza masomo yao katika Shule hii nimefurahishwa na kiwango cha elimu kinachotolewa shuleni hapa pamoja na juhudi zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na uwezo wa kuwasiliana kwa ujasiri”
Naye Diwani wa Kata ya Gangilonga, Kenyata Likotiko amelipongeza Kanisa Katoliki kwa uwekezaji katika sekta ya elimu kupitia shule za St. Dominic, akisema uwekezaji huo umekuwa chachu ya maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na umeongeza imani ya wazazi katika shule hizo.
“Nampongeza Padre Ulungi kwa kutimiza miaka 30 ya huduma katika Jimbo la Iringa katika kipindi hicho amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu na jamii,kuanzia kuanzishwa na kuendelezwa kwa shule za St. Dominic ikiwemo matawi yaliyopo maeneo mbalimbali kumechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla”
Aidha kwa upande wake Mchungaji wa kanisa la kiinjilisti la kilutheri Dayosisi ya Iringa Yusto Jaffet Kinyowa amewataka wazazi na walezi nchini kuendelea kuziamini shule hizo kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kuwajengea vijana maarifa na msingi mzuri wa maisha alisema elimu inayotolewa katika shule hizo huwasaidia wanafunzi kuendeleza maarifa waliyoyapata katika elimu ya msingi na kuwaandaa kwa masomo ya juu na maisha ya baadaye.
“Shule hizi zinatoa mafunzo ya ziada yanayowajengea wanafunzi uwezo wa kuwasiliana na kujifunza lugha mbalimbali, ikiwemo lugha ya Kichina, stadi hizi ni muhimu kwa vijana katika dunia ya sasa na zinaweza kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za kielimu na kiuchumi pia niwashukuru wazazi, walezi, walimu na wanafunzi kwa mchango wao katika kufanikisha elimu, akisisitiza kuwa kuwekeza katika elimu ya msingi na sekondari ni kuwekeza katika taifa la kesho”




