Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
THAMANI YA BIDHAA HOROHORO YA PANDA NA KUGUSA  SH.BILIONI 548

THAMANI YA BIDHAA HOROHORO YA PANDA NA KUGUSA SH.BILIONI 548

 

NA AMINA SAIDI,

MATUKIO DAIMA,TANGA.

 BIASHARA kati ya Tanzania na Kenya imeendelea kuimarika kwa kasi kubwa, huku thamani ya bidhaa zinazoingia nchini kupitia Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani (OSBP) cha Horohoro mkoani Tanga ikiongezeka  kutoka Sh. bilioni 306.4 katika mwaka wa fedha 2022/23 hadi kufikia Sh. bilioni 548.8 mwaka 2024/25.


 Hatua hii kubwa inadhihirisha kukua kwa kasi kwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizi mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


​Mwenendo huo mzuri wa kibiashara ulibainishwa na Afisa Mfawidhi wa Kituo hicho, Shadrack Mbonea Kavuta, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa EAC,  Annet Semwamba.

 Kiongozi huyo alikuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea mpaka huo ili kujionea mafanikio na ufanisi uliopatikana kupitia mfumo wa huduma za pamoja mpakani.


​Kavuta alieleza kuwa kasi hiyo ya ukuaji imeendelea kushika kasi katika mwaka wa fedha wa sasa wa 2025/26 ambapo hadi sasa thamani ya bidhaa zilizoingia kupitia kituo hicho imeshafikia Sh. bilioni 489.5. Ongezeko hili linalenga kuweka rekodi mpya ya kibiashara na kudhihirisha kuwa mpaka huo umekuwa kiungo muhimu cha kukuza uchumi wa pande zote mbili.


​Kwa upande wa mauzo ya nje, thamani ya bidhaa zilizotoka nchini kwenda Kenya kupitia kituo hicho nayo imerekodi ukuaji wa kuridhisha.


 Takwimu zinaonyesha kuwa mauzo hayo yameongezeka kutoka Sh. bilioni 134.7 katika mwaka wa fedha 2022/23 hadi kufikia Sh. bilioni 175.9 katika mwaka wa fedha 2025/26.


Mafanikio haya makubwa yanachangiwa na ushirikiano thabiti uliopo kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA).


​Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo ya kupigiwa mfano, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa zinazotishia ufanisi wake wa kazi.


 Kavuta alitaja changamoto kubwa kuwa ni ukosefu wa umeme wa uhakika na uhaba wa vifaa vya kuzimia moto. Kutokana na hali hiyo, aliiomba Sekretarieti ya EAC kusaidia kuboresha miundombinu hiyo ili kuimarisha usalama wa kituo na kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na majanga.


​Kituo cha Horohoro sasa kinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kikiwa kimeunganisha taasisi 19 za kiserikali zinazotoa huduma chini ya paa moja, zikiratibiwa na TRA. 

Taasisi hizo ni pamoja na Idara ya Uhamiaji, Polisi, JWTZ, TMDA, TPHPA, TFS, TAWA, Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

 


Muundo huu unasaidia kuondoa urasimu na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka.

​Kazi kubwa zinazofanywa na taasisi hizo kwa pamoja ni pamoja na kukusanya mapato ya serikali, kurahisisha biashara za mipakani, na kulinda jamii dhidi ya uingizaji wa bidhaa hatarishi.


 Aidha, kituo hicho kinalenga kusimamia utekelezaji wa sera na mikataba ya kimataifa ya biashara, kukusanya takwimu sahihi, pamoja na kudhibiti vitendo vya magendo mipakani.


​Akijibu taarifa hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Bi. Annet Semwamba, alieleza kuridhishwa kwake na mafanikio yaliyopatikana Horohoro na kupongeza weledi wa watumishi wa mpaka huo.


 Alihitimisha kwa kuahidi kuwa Sekretarieti ya EAC ipo tayari kushirikiana na wadau wote kutatua changamoto zilizowasilishwa, lengo likiwa ni kuendelea kuimarisha mtengamano na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3