MIGOGORO WANANCHI, HIFADHI YA KAGERANKANDA YAANZA KUPATIWA UFUMBUZI
Banyikwa Makinga Mtendaji wa kata ya KageraNkanda halmashauri ya wilaya Kasulu mkoani Kigoma
Batro Ngilangwa Mratibu wa mradi wa uhifadhi Shirikishi hifadhi ya Msitu KageraNkanda kutoka Shirika la TAWEA
Patrick Emilian Meneja wa shamba la miti la Hifadhi ya Msitu wa KageraNkanda halamshauri ya wilaya Kasulu mkoani Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Uhasama na mahusiano duni baina ya wananchi na hifadhi ya msitu wa Makere Kusini Maarufu KageraNkanda wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma yameanza kujengwa upya kufuatia utekelezaji wa mradi wa uhifadhi shirikishi ambao unawaweka pamoja wananchi wa vijiji vinne vinavyozunguka eneo hilo na mamlaka za usimamizi wa misitu na wanyamapori.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa siku mbili wa wadau wa uhifadhi shirikishi kuzungumzia utekelezaji wa mpango huo unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Wote Equality Alliance (TAWEA) ambapo shughuli za kiuchumi nje ya maeneo ya hifadhi zimeanzishwa.
Akizungumza katika mkutano huo Mratibu wa mradi wa Uhifadhi Shirikishi kutoka TAWEA, Batro Ngilangwa alisema kuwa kwa mwaka mmoja sasa tangu mradi huo uanze kutekelezwa ipo miradi ya kiuchumi iliyoanzishwa kwa wananchi ikiwamo mradi wa ufugaji samaki kwenye mabwawa, ufugaji nyuki na urinaji asali, kilimo mseto na uanzishwaji wa vikundi vya akiba na mikopo miradi ambayo imeondoa utegemezi wa kiuchumi wa wananchi kwenye hifadhi ya Msitu ya KageraNkanda.
Akizungumza katika mkutano huo Meneja wa Shamba la miti la Buhigwe/Makere , Patrick Emilian alisema kuwa kupitia mradi huo wanaamini mahusiano yao na wananchi wa vijiji hivyo yataimarika na kushirikiana kufanya shughuli za uhifadhi, miradi ya kiuchumi ya wananchi na kujenga mustakabali wa pamoja baina ya pande hizo huku utekelezaji wa sheria za uhifadhi zikitekelezwa kwa uelewa wa pamoja.
Naye Afisa Mtendaji wa kata ya KageraNkanda, Makinga alisema kuwa awali kulikuwa na changamoto kubwa ya mahusiano baina ya Watendaji wa TFS,TAWA na mamlaka za uhifadhi dhidi ya uongozi wa vijiji,kata na wnanchi ambapo maafisa hao walikuwa wakiingia kwenye vijiji vyao kukamata wahalifu na kufanya opereshani bila kutoa taarifa kwa uongozi wa vijiji hivyo kunatokea upinzani unaokwamisha kufanya shughuli zao.
Mwisho.





