DARAJA LA NANYUMBU KUIMARISHA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA KIJAMII KIJIJI CHA MBANGALA WILAYANI NANYUMBU
Jul 2, 2026
Nanyumbu, Mtwara
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE programu ya uondoaji vikwazo vya barabara (Bottleneck) imekamilisha ujenzi wa daraja la mawe katika barabara ya Nyumbu-Mbangala Mbuyuni wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.
Kukamilika kwa mradi huo kumeondoa kikwazo cha muda mrefu kwa wakazi wa kijiji cha Mbagala na vijiji vya jirani kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya hivi karibuni iliyofanywa na timu ya Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA iliyotembelea miradi ya RISE inayotekelezwa katika wilaya hiyo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Meneja wa TARURA wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Dikson Mkokota amesema wametumia kiasi cha shilingi milioni 195 kwa ajili ya ujenzi wa boksi kalavati la mawe ili kuondoa kikwazo kilichokuwepo katika barabara ya Nanyumbu kuelekea Mbangala Mbuyuni.
"Hili eneo lilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa sababu maji yalikuwa yanakatisha kwenye barabara na kuzuia watu kutoka upande wa Mbangala Mbuyuni kuelekea Nanyumbu kwa ajili ya kupata huduma za kijamii", amesema Mhandisi Dikson Mkokota.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mkokota ujenzi wa daraja hilo umesaidia kuondoa kikwazo katika barabara hiyo huku akitolea mfano wa urahisi wa usafirishaji wa mazao ambapo sasa yanaweza kusafirishwa kutoka kijiji cha Mbangala Mbuyuni kuelekea Nanyumbu na Mangaka ambako kuna Maghala makubwa.
Ameelezea manufaa mengine ya mradi huo kijamii ni pamoja na kuwarahisishia wakazi wa Mbangala Mbuyuni kuzifikia huduma za afya na elimu zinazopatikana kituo cha afya Nanyumbu na shule ya sekondari Nanyumbu katika Kijiji cha Nanyumbu.
Kwa upande wake, Bw. Marijani Mohamed mkazi wa Mbangala Mbuyuni amesema ujenzi wa daraja hilo umewapa unafuu wa maisha kwani hapo awali walilazimika kuzunguka kijiji jirani ili kufika Nanyumbu kwaajili ya kupata mahitaji yao ya kila siku hali iliyowasababishia si usumbufu tu bali hata gharama zilikuwa kubwa.
TARURA inatekeleza programu ya kuondoa vikwazo vya barabara (bottleneck) hususani maeneo ya vijijini kupitia mradi wa RISE ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii ili kuleta tija katika maeneo husika na hata taifa kwa ujumla.

