Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MZEE KAYUMBA: MATUMIZI YA BIDHAA ZA NDANI NI CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA

MZEE KAYUMBA: MATUMIZI YA BIDHAA ZA NDANI NI CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA


Na Hamida  Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuchochea maendeleo ya uchumi na kuunga mkono juhudi za vijana wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia ujuzi wanaoupata katika vyuo vya ufundi stadi.

Hayo yamesemwa na mkazi wa Dodoma, Mzee Kayumba, baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Chinangali Park jijini Dodoma.

Mzee Kayumba amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa na VETA pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi, akieleza kuwa bidhaa hizo zinaonesha ubunifu mkubwa, umahiri wa hali ya juu na uwezo wa vijana wa Kitanzania kutumia maarifa yao kuzalisha bidhaa bora.

Amesema alichokiona katika banda la VETA kinathibitisha kuwa taasisi hiyo inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwajengea vijana uwezo wa kiufundi unaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

"Nimefurahishwa sana na kazi zinazofanywa na vijana hawa. Bidhaa nilizoziona zina ubora mkubwa na zinaonesha wazi kuwa vijana wa Kitanzania wana uwezo wa kutengeneza vitu vizuri na vinavyovutia endapo watapatiwa mafunzo na mazingira sahihi ya kufanya kazi," amesema.

Aidha, amesema VETA inapaswa kuendelea kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wengi zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma.

Kwa mujibu wake, maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa kutegemea bidhaa kutoka nje pekee, bali yanahitaji uwekezaji katika uzalishaji wa ndani pamoja na matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa na Watanzania wenyewe.

Aongeza kuwa bidhaa zinazozalishwa na vijana wa Kitanzania zina ubora unaostahili kuaminiwa na kutumiwa na wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo wa kudharau bidhaa za ndani.

"Ni wakati wa Watanzania kuamini uwezo wao wenyewe tunapaswa kutumia bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini kwa sababu kufanya hivyo kunasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuwapa motisha vijana wanaotumia ujuzi wao kuzalisha bidhaa mbalimbali," amesema.

Mzee Kayumba pia alitoa wito kwa wazazi na vijana kutembelea mabanda ya VETA katika maonesho hayo ili kujifunza kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mafunzo ya ufundi stadi na kujionea kazi zinazofanywa na wanafunzi wa vyuo hivyo.

Amesema elimu ya ufundi stadi ni miongoni mwa suluhisho muhimu la changamoto ya ajira kwa vijana kwani huwapa maarifa na stadi zinazowawezesha kujiajiri, kuanzisha biashara zao na hata kuajiri wengine.

Aidha, amehimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika vyuo vya VETA kupata mafunzo yatakayowawezesha kuwa wabunifu, wazalishaji na wachangiaji wakubwa wa maendeleo ya taifa.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3