Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WATANZANIA NA TAASISI MBALIMBALI WATAKIWA KUCHANGIA MFUKO WA MATIBABU YA UROTO NA FIGO BMH

WATANZANIA NA TAASISI MBALIMBALI WATAKIWA KUCHANGIA MFUKO WA MATIBABU YA UROTO NA FIGO BMH

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


WATANZANIA, Taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kuchangia Mfuko wa Kusaidia Matibabu ya Uroto na Figo uliozinduliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), wenye lengo la kukusanya Sh bilioni 7 ndani ya miaka miwili kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kibingwa nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema mfuko huo umeanzishwa kutokana na gharama kubwa za matibabu ya upandikizaji figo na uroto ambazo bado ni changamoto kwa wagonjwa wengi nchini.


Amesema BMH imeendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa na sasa imekuwa tegemeo kwa zaidi ya Watanzania milioni 10 wanaopata huduma mbalimbali za afya ndani ya nchi.


Senyamule amesema mafanikio yaliyofikiwa na hospitali hiyo yanaonesha uwezo mkubwa wa kutoa huduma ambazo hapo awali zilikuwa zikipatikana nje ya nchi pekee.


Amesema huduma za upandikizaji figo sasa zinapatikana nchini ambapo zaidi ya wagonjwa 55 tayari wamefanikiwa kupandikizwa figo, huku watoto 28 wakifanyiwa upandikizaji wa uroto, hatua ambayo ameielezea kama mafanikio makubwa kwa sekta ya afya.


Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa rasilimali fedha ili kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma hizo muhimu za kibingwa.


Kutokana na hali hiyo, amewataka Watanzania, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo kujitokeza kuchangia mfuko huo ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji.


Amesema kila mchango, mkubwa au mdogo, unaweza kuwa chanzo cha kuokoa maisha ya mgonjwa.


Aidha, Mkoa wa Dodoma umeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za BMH, ukisema zimeiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk. Henry Humba, alisema maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za kibingwa nchini.


Amesema huduma za upandikizaji figo na uroto ni za gharama kubwa, hivyo mfuko huo umeanzishwa ili kusaidia wananchi wenye uhitaji kupata matibabu kwa urahisi zaidi.


“Maadhimisho haya ni sehemu ya kuunga mkono Serikali katika kuhakikisha huduma za kibingwa zinaimarishwa zaidi,Kupitia hatua hii tunataka kuendeleza na kupanua jitihada zilizokwishaanzishwa,” amesema Dk. Humba.


Ameongeza kuwa hospitali hiyo imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na maendeleo kuhakikisha mfuko huo unafanikiwa, huku akisisitiza kuwa changamoto zilizopo hazipaswi kuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma.


Aidha,amebainisha kuwa mchango wa awali wa Sh bilioni 1 uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma hizo za kibingwa nchini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3