WANAWAKE WABEBESHWA MZIGO MKUBWA WA ATHARI ZA MAZINGIRA
May 8, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
ASLIMIA 81 ya kaya za vijijini nchini bado hutegemea kuni kwa shughuli za kupikia, hali inayowaongezea wanawake mzigo mkubwa wa kazi za mazingira pamoja na kuathiri afya zao na muda wao wa uzalishaji.
Hayo yamebainishwa katika Utafiti wa Jinsia na Mazingira wa mwaka 2025 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ambao pia umeonyesha kuwa wanawake wanaendelea kubeba sehemu kubwa ya kazi zisizo na malipo zinazohusiana na mazingira ikilinganishwa na wanaume.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Tafiti za Uwezeshaji wa Wanawake na Lishe za mwaka 2023/24 pamoja na Utafiti wa Jinsia na Mazingira wa mwaka 2025, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisema hali hiyo pia inachangia kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira.
Alisema wakati wanawake wakijihusisha zaidi na kazi za mazingira zisizo na malipo, wanaume wengi hujihusisha na shughuli zenye kipato, jambo ambalo linaendelea kuongeza tofauti za kiuchumi kati ya jinsia hizo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake pia wameonekana kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi ambapo asilimia 82.9 walikumbwa na angalau athari moja ya tabianchi ikilinganishwa na asilimia 80.8 ya wanaume Tanzania Bara.
Aidha, ukame umetajwa kuwa changamoto kubwa zaidi hasa katika maeneo ya vijijini na nyanda kame, ambapo umeathiri asilimia 50 ya kaya katika maeneo hayo.
Dk. Gwajima alisema pamoja na Watanzania wengi kufahamu athari za mabadiliko ya tabianchi, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa taarifa za tahadhari ya majanga, hasa kwa wanawake.
Alisema katika maeneo ya pwani, wanawake waliopokea taarifa za onyo la mapema kuhusu majanga walikuwa asilimia 16.6 pekee ikilinganishwa na asilimia 21.8 ya wanaume.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, matokeo ya utafiti huo yanapaswa kuwa chachu ya kuchukua hatua mahsusi katika kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa, utunzaji wa mazingira pamoja na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Mwisho





