Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 RIDHIWANI:HAKUTAKUWA NA MABADILIKO YA VITUO VYA KAZI KWA WAAJIRIWA WAPYA

RIDHIWANI:HAKUTAKUWA NA MABADILIKO YA VITUO VYA KAZI KWA WAAJIRIWA WAPYA

  

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

SERIKALI imetangaza kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya vituo vya kazi kwa waajiriwa wapya waliopata ajira katika zoezi la ajira 12,000, ikieleza kuwa nafasi hizo zilitolewa kulingana na mahitaji halisi ya kila Halmashauri na mwajiri husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,kuhusu ahadi za Siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema kuruhusu mabadiliko ya vituo vya kazi kutasababisha upungufu wa watumishi katika maeneo yaliyopangiwa na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ridhiwani amesema Serikali imefanya upangaji wa ajira hizo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kila Halmashauri inanufaika kulingana na uhitaji wake, hivyo waajiriwa wapya wanapaswa kwenda kufanya kazi katika vituo walivyopangiwa bila masharti.

Amesisitiza kuwa waajiriwa wote wapya wanapaswa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 tangu kupokea barua za ajira, akionya kuwa watakaokiuka utaratibu huo watapoteza nafasi zao ambazo zitachukuliwa na waombaji wengine waliopo kwenye kanzi data ya Sekretarieti ya Ajira.

Aidha, Waziri huyo amewaelekeza waajiri wa Serikali kuhakikisha kuwa baada ya kuwapokea waajiriwa wapya, wanawasilisha taarifa zao kwa Mhariri Mkuu wa Gazeti la Serikali ili ajira hizo zichapishwe rasmi kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma.

Katika hatua nyingine, Ridhiwani amewahimiza vijana wenye sifa kuendelea kuomba ajira pindi nafasi zitakapotangazwa, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ajira kulingana na mahitaji ya sekta mbalimbali nchini.

Alifafanua kuwa mbali na ajira 12,000 zilizoanza kutekelezwa, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia pia kibali cha ajira 41,500 kwa kada mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, uvuvi, uhandisi na sekta za ulinzi na usalama.

Waziri huyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025 inayolenga kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuimarisha Utumishi wa Umma kama nguzo ya utawala bora.

Ridhiwani ameeleza kuwa Serikali imeboresha mfumo wa e-Mrejesho kwa kuongeza dirisha la “Sema na Kiongozi” linalowawezesha wananchi kuwasilisha moja kwa moja malalamiko, maoni na mapendekezo yao kwa viongozi wa Serikali.

Kupitia mfumo huo, viongozi wa ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya wanapata fursa ya kufuatilia na kutoa maelekezo kuhusu malalamiko ya wananchi, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa huduma za umma.

Ameongeza kuwa wananchi wanaweza kutumia tovuti ya e-Mrejesho, programu ya simu au huduma ya USSD bila gharama, jambo linalowezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika utoaji wa mrejesho kwa Serikali.

Hata hivyo Serikali itaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais kwa vitendo, kwa lengo la kuboresha utumishi wa umma, kuongeza ajira kwa vijana na kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na huduma zinazotolewa na Serikali.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3