MADIWANI MBOZI WAONYWA KUHUSU MGONGANO WA MASLAHI, MATUSI NA ULEVI
Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, wamekumbushwa kuviishi viapo vyao, ikiwamo ahadi ya Uadilifu, kwa kusimamia majukumu yao bila kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha mgongano wa maslahi, ambavyo vimetajwa kuwa chanzo cha kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rai hiyo ilitolewa Disemba 5, 2025 na Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Majid Mohamed, wakati madiwani hao wakiahidi kutekeleza kiapo chao mara baada ya kuapishwa katika mkutano wa kwanza wa baraza hilo.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Vwawa Day, wilayani humo, na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na watendaji wa Halmashauri, wakiwemo wananchi kutoka kata mbalimbali.
Mohamed alisema madiwani hawapaswi kushiriki au kujihusisha kwa namna yoyote na zabuni zinazotangazwa na Halmashauri, kwani kufanya hivyo kunahatarisha uwazi na haki .
Aidha, aliwakumbusha kuwa zawadi wanazopokea baada ya kuwahudumia wananchi hazipaswi kuzidi kiasi cha shilingi 200,000, na endapo zitazidi kiwango hicho wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi ili ziwekwe kwenye mpango rasmi wa matumizi.
Baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la kiapo, Madiwani wa Halmashauri hiyo, wamemchagua kwa kishindo Diwani wa Kata ya Halungu, Maarifa Mwashitete, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, akiibuka na kura zote 40.

.jpeg)
.jpeg)