Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
KIOO LIMITED YATOA MSAADA WA VIFAA VYA TSH MILIONI 150 SHULENI MKURANGA

KIOO LIMITED YATOA MSAADA WA VIFAA VYA TSH MILIONI 150 SHULENI MKURANGA

Na Matukio Daima Media

KAMPUNI ya KIOO Limited imetoa misaada mbalimbali kwa shule za Msingi na Sekondari Mkuranga Mkoa wa Pwani zinazofikia shilingi milioni 150 kwa mwaka jana kama sehemu ya mpango wake wa kusaidia jamii wa (Cooperate Social Responsibility (CSR).

Mwishoni mwa wiki kampuni hiyo ilikabidhi mashine za kurudufia karatasi na kompyuta kwa shule za sekondari za Msorwa na Malela zilizoko Wilaya ya  Mkuranga Mkoa wa Pwani zenye thamani y ash milioni nane.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa mwishoni mwa wiki na Mshauri wa Masuala ya Usalama, Afya na Mazingira wa Kioo Limited, Richard Msumule, wakati wa hafla iliyohudhuriwa na Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Jessy Mpangala.


Akizungumza mara baada ya kutoa msaada huo, Richard Msumule alisema katika mpango wake wa CSR, Kioo Limited imekuwa ikikarabati madarasa, ofisi za walimu na  kujenga visima vya maji.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikiwajengea miradi ya nishati safi ya gesi, majiko ya gesi, kuwanunulia kompyuta na kujenga madarasa mapya kwa shule mbalimbali za Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Ofisa Elimu Wilaya ya Mkuranga, Jessy Mpangala aliipongeza kampuni ya Kioo Limited kwa namna ambavyo imekuwa ikizisaidia mara kwa mara shule zilizopo katika Wilaya hiyo vifaa mbalimbali.


Alisema kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada ya aina mbalimbali ikiwemo kukarabati madarasa na ofisi za walimu, kuchimba visima vya maji, kununua madawati na kukarabati ofisi za walimu wa shule hizo.

“Kwa dhati kabisa napenda kuwapongeza na kuwaambia kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wenu ambao umekuwa endelevu kwa shule zetu hapa Mkuranga, mmekuwa mkitatua changamoto mbalimbali kila mnapoambiwa hongereni sana,” alisema Ofisa Elimu


“Mnajua serikali haiwezi kufanya kila kitu kwa kuwa inahudumia shule nyingi sana na mahitaji ni makubwa kwa hiyo msichoke kutusaidia kila viongozi wa vijiji na kata wanapowafuata kuwaeleza shida za vitu mbalimbali kwenye shule, zahanati na ofisi za vijiji,” alisema

Naye Richard alisema KIOO  Limited kila mwaka imekuwa ikitenga mafungu ya fedha kwaajili ya kutoa shukrani kwa jamii kama sehemu ya mpango wake wa CSR

Alisema wamekuwa wakiletewa mapendekezo ya miradi ya kufadhili kutoka kwa viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakipata maoni kutoka kwa wananchi wao kuhusu vipaumbele vyao.

“Sisi huwa tunasikiliza viongozi wa vijiji wanakaa wanazungumza na wananchi wao wanakubaliana kwamba kipaumbele ninini kisha wanakuja kwetu na sisi tunaangalia uwezo wetu kisha tunatekeleza,” alisema na kuongeza

“Kwa hiyo miradi yote ambayo tunafadhili ukiwemo wa gesi kwenye shule ya sekondari Vianzi ni miradi ambayo iliibuliwa na viongozi wenyewe sisi hatuamui tusaidia kitu gani ila wao ndio wanaamua na kutuletea mapendekezo kwetu,” alisema Richard

Richard alisema kwa mwaka 2026 Kioo Limited imepanga kufadhi miradi kadhaa kwenye kijiji cha Msorwa ikiwemo kituo cha afya Msorwa, kukarabati kisima katika shule ya msingi Msorwa, kununua mashine ya kudurufia kwa shule ya sekondari Msorwa.


Alisema Kioo Limited imepanga kununua vitanda viwili katika kituo cha afya Msorwa na kukarabati madarasa mawili na ofisi za walimu kwenye shule msingi Msorwa.

Alisema katika kijiji cha Malela wanatarajia kukarabati madarasa mawili katika shule ya msingi malela, kuinunulia kompyuta mpakato shule ya sekondari Malela, kununua mashine ya kudurufia, kukarabati madarasa mawili shule ya sekondari Malela na kukarabati ofisi ya Malela.

Alisema Kioo Limited imepanga kuongeza matundu sita ya vyoo  na kukarabati madarasa manne kwa shule ya sekondari Vianzi iliyoko wilayani humo.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3